Ugiriki kurudia uchaguzi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Majengo ya bunge nchini Ugiriki

Baada ya juhudi za kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kukwama nchini Ugiriki sasa nchi hiyo itarudia uchaguzi June 17 na Jaji Panagiotis Pikramenos ameteuliwa kuongoza serikali ya mpito hadi uchaguzi utakapofanyika.

Siku ya uchaguzi imetajwa baada ya viongozi wa vyama kukutana na Rais wa nchi hiyo Karolos Papoulias.

Kumekuwa na hali ya sintofahamu nchini Ugiriki baada ya uchaguzi kuhusu suala la kubana matumizi kama lisiendelee au liendelee kama makubaliano ya kimataifa ambayo yanaitaka nchi hiyo kunusuru uchumi kwa kukopa fedha.

Katika matokeo ya kura ya maoni ya hivi karibuni, chama cha Syriza cha mrengo wa kushoto ambacho kinapinga mpango huo wa kubana matumizi kimetabiriwa kuwa kinaweza kushinda uchaguzi huo wa marudio, lakini hakitaweza kupata viti vya bunge vya kutosha kuunda serikali.

Mvutano uliokuwa unaendelea nchini Ugiriki pia umeleta athari katika ukanda wa euro ambapo pia imesababisha sarafu ya euro kushuka dhidi ya dola ya marekani .

Kumekuwa na wasi wasi kuhusu mstakabali wa baadae wa Ugiriki katika Umoja wa Ulaya ambapo maafisa wa Umoja wa Ulaya wana hofu kwani kama Ugiriki itachagua chama kinachopinga mpango wa kubana matumizi na kukopa fedha za kunusuru uchumi hilo litaifanya Ugiriki kujiondoa katika ukanda unaotumia sarafu ya Euro.