17 wahukumiwa kifo na jeshi-Somaliland

Mahakama moja ya kijeshi mjini Hargeisa, mji mkuu wa nchi iliyojitangaza kua huru ya Somaliland, imewahukumu watu 17 adhabu ya kifo kwa kushambulia kambi ya jeshi.

Hukumu hizo zimetolewa siku moja baada ya tukio hilo la uvamizi ambapo watu saba waliuawa, kwa mujibu wa msemaji wa Somaliland aliyezungumza na BBC.

Kundi lililokua na silaha lilifanya shambulio hilo likidai kua jeshi lilijenga kambi hio kwenye ardhi ambayo wao walimiliki kwa vizazi vingi.

Haki miliki ya picha Other
Image caption Ramani ya Somaliland

Nchi ya Somaliland imejiepusha ghasia na vurugu zilizoko nchini Somalia.

Kundi la hadi watu 30 kutoka ukoo mmoja wakiwa na silaha, mnamo siku ya Ijumanne walivamia kambi wakisababisha mapambano ya kutumia silaha ambamo watu watatu waliuawa, Waziri wa Somaliland wa ulinzi Ahmed Haji Ali aliiambia idhaa ya Kisomali ya BBC.

Baada ya kukamatwa watu 28 walitiwa korokoroni usiku kucha -na kufikishwa mbele ya mahakama ya kijeshi asubuhi.

Miongoni mwa washambuliaji hao walikuemo vijana saba walio chini ya umri wa kuhukumiwa, lakini wamepewa kifungo cha maisha.

Watatu waliachiliwa, huku kesi ya wengine watatu ikiahirishwa kwa sababu walijeruhiwa wakati wa shambulio.

Endapo hukumu hii itafanyika kwa mauwaji ya watuhumiwa, inaweza kuzusha ghasia zaidi kutoka kwa wana ukoo wa hao waliohukumiwa, kwa mujibu wa mwanmdishi wa BBC.

Mwandishi wetu Mohamed Mohamed anasema kua suala la ardhi nchini Somaliland ni tatizo sugu na linatokea mara kwa mara.

Image caption Utawala wa Somaliland

Somaliland ilijitangazia uhuru mnamo mwaka 1991 baada ya mapinduzi yaliyomtoa madarakani Rais Siad Barre.

Ni nchi ambayo ina utulivu na ina tabia ya kufanya uchaguzi wa viongozi wake mara kwa mara.