Mateka Mjerumani auawa Nigeria

Image caption Mhandisi wa Kijerumani alitekwa nyara huko Kano

Mhandisi wa Kijerumani aliyetekwa mwezi Januari mwaka huu kaskazini mwa Nigeria ameuawa katika jaribio la kumuokoa lililotibuka.

Rubaa za usalama zinasema mhandisi huyo aliuawa na watekaji nyara wake. Mhandisi huyo Edgar Fritz Raupach alitekwa nyara katika eneo la Kano.

Hapo mwezi machi mateka wawili raia wa Uingereza na Italia waliuawa katika jaribio sawa na hilo lililofanywa na wanajeshi wa Uingereza na Nigeria.

Matukio ya sasa yanajiri wakati maafisa wa Italia wakisema mhandisi wa Kitaliano ametekwa nyara magharibi mwa Nigeria.

Utekaji nyara si jambo la kawaida katika jimbo la Kwara. Hata hivyo wafanyikazi wa mafuta wamekuwa wakilengwa na makundi yanayodai kikombozi kusini mwa Nigeria huku Kaskazini usalama mbaya unashuhudiwa kutokana na harakati za kundi la kiisilamu.

Mwandishi wa BBC nchini Nigeria Will Ross amesema tukio la sasa ni ishara kwamba maafisa wa usalama Nigeria wameshindwa kuzuia utekaji nyara wa wageni, na pia hatari iliyoko katika jaribio la kuwaokoa mateka.

Serikali ya Ujerumani imesema inaanza kuchunguza matukio yaliyosababisha kifo cha raia wake.