Walker ashinda uchaguzi wa ghafla

Raia wa Wisconsin wakisherekea ushindi wa Republican Haki miliki ya picha AP
Image caption Raia wa Wisconsin wakisherekea ushindi wa Republican

Gavana wa chama cha Republican wa jimbo la Wisconsin, nchini Marekani, Scott Walker, amekuwa gavana wa kwanza katika historia ya Marekani, kunusurika jaribio la kumuondoa madarakani.

Mpinzani wake, Tom Barret wa chama cha Democrat, ambaye alimshinda mwaka wa 2010 amekubali kushindwa.

Walker alichochea ghadhabu miongoni mwa raia wa jimbo hilo kwa kuidhinisha sheria mpya kuhusu haki za vyama vya wafanyakazi na pia kuwalazimisha wafanyakazi wa umma kuchangia zaidi katika hazina yao ya malipo ya uzeeni.

Mwandishi wa BBC mjini Washington, anasema ushindi huo wa Bwana Walker, utailazimisha chama cha Democratic, kuongezea maradufu hazina yake ya kampeini katika jimbo hilo, ambalo limekuwa likiunga mkono wagombea wa urais wa chama cha Democratic tangu mwaka wa 1988.