Zaidi ya watu 78 wadaiwa kuuawa Syria

Syria Haki miliki ya picha 1
Image caption Syria

Wanaharakati wa upinzani nchini Syria, wamedai kuwa wanajeshi wa serikali wamewaua takriban watu 78 wakiwemo kina mama na watoto, katika mkoa wa Hama.

Wanaharakati hao wanasema mauaji hayo ni sawa na mauaji mengine ya halaiki yaliyotekelezwa na wanajeshi ha mjini Houla.

Wanaharakati hao wanasema wanajeshi wa waasi wanaounga mkono serikali na wale wa serikali walishambulia kijiji cha Qubeir, huku wakiwafyatulia risasi raia kwa karibu na kuwadunga visu hadi kufa.

Wanasema waliouawa zaidi ni kina mama ishirini na watoto ishirini.

Lakinio runinga ya taifa nchini humo imesema kuwa maafisa wa ulinzi waliwavamia magaidi mjini Qubeir kufuatia wito kutoka kwa raia wa eneo hilo.

Manusura waelezea zaidi

Mmoja wa manusura wa shambulio hilo, ameiambia BBC kuwa, wakati wanamgambo hao wa waasi na wale wa serikali walipoondoka mjini humo, tayari alikuwa amegundua miili arubaini.

Amesema nyingi zilikuwa za kina mama na watoto ambao walikuwa wameuawa kwa kudungwa visu.

Mmoja wa waathirika ni mtoto mmoja mwen ye umri wa miezi mitatu, ambaye mwili wake ulikuwa umechomwa.

Amesema watu 4 kutoka kwa familia yale waliuawa kwenye tukio hilo.

Wengi wa waliofanya uvamizi huo wanasemekana kutoka vijiji vinne jirani ambavyo vinajulikana kuwa ngome ya serikali.

Mtu huyo amesema kuwa aliwapigia simu wachunguzi wa Umoja wa Mataifa zaidi ya mara kumi waje wajionee, lakini walimfahamishwa kuwa watazuru eneo hilo pindi tu watakapopata idhini ya serikali.

Hata hivyo madai hayo hayajathibitishwa.

Annan ataka mataifa zaidi yashirikishwe

Wakati huo huo, mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria, Kofi Annan, anapanga kutoa mapendekezo mapya ili kufufua mpango wake wa amani ambao unaonekana kusambaratika nchini Syria.

Mabalozi wanasema, Annan, anatarajiwa kulishawishi baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuanzisha majadiliano na makundi mapya kukiwemo wanachama wa kudumu wa baraza hilo na Iran ili kujaribu kumaliza ghasia zinazoendelea kushuhudiwa nchini Syria.

Mpango huo unadhamiria kuimarisha mikakati ya kumaliza ghasia na kuanzisha mageuzi ya kisiasa na kubuni serikali ya mpito.

Pendekezo hilo limetolewa na Urussi, lakini mataifa ya Marekani, Uingereza na Ufaransa yamekataa wazo la kujumuisha Iran, katika kundi lolote linashughulika na mzozo huo wa Syria.