Annan ataka dunia iungane dhidi ya Syria

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Kofi Annan Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Kofi Annan

Ujumbe maalumu wa Bwana Koffi Annan kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ulikuwa kwamba Baraza hilo ni sharti liungane katika hatua ya kushinikiza Serikali ya Syria kutekeleza mpango wake, au sio hali hiyo itasababisha hali kuwa mbovu zaidi.

Bwana Annan, ambaye ni balozi maalumu wa maswala ya Syria, kwa mara ya kwanza aligusia uwezekano wa kutumia vikwazo, akisisitiza kuwa lazima kuwepo na adhabu ya aina fulani kwa ye yote anayekataa kufuatilia kikamilifu mpango huo wa amani.

Katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kulikuwepo mapatano ya kauli moja kuwa lazima hatua muhimu ichukuliwe lakini, ingawa haikubainika hatua ipi inapaswa kuchukuliwa.

Mataifa kadhaa ya Magharibi yalipendekeza vikwazo lakini Urusi ililipa wazo hilo kisogo na kutoa kauli kuwa makundi ya upinzano yenye silaha yasiposhinikizwa pia hakuna haja ye yote kwa Serikali kukubali mapendekezo ya jamii ya kimataifa.

Wakati huohuo Bwana Annan alikiri kuwa mashauriano yameanza juu ya uwezakano wa kuanzisha jopo la eneo na viongozi wa kimataifa ili kushawishi Serikali ya Syria kupunguza uhasama kati yao.