Uspania yahitaji dola bilioni 50 zaidi

Shirika la Fedha Duniani, IMF, linasema kuwa mabenki ya Uspania yanahitaji fedha kama dola bilioni 50 zaidi.

Haki miliki ya picha BBC World Service

Uspania inatarajiwa leo kuomba rasmi mkopo kutoka mfuko wa msaada wa nchi zinazotumia sarafu ya euro.

Awali serikali ilisema inasubiri tathmini ya wataalamu wa hesabu kuhusu mabenki ya nchi hiyo, lakini mwandishi wa BBC mjini Madrid anasema, Uspania inahimizwa kuchukua hatua haraka.

Mabenki ya Uspania yamekabwa na mikopo yaliyotoa kwa watu walionunua nyumba, huku bei za majengo zimeporomoka.

Mkuu wa IMF amesema ni muhimu kwa mabenki ya Ulaya kusawazishwa, ili uchumi wa dunia utengenee.

Akizungumza mjini New York, Christine Lagarde alisema ingawa miaka mitano imepita tangu msukosuko wa kiuchumi kuanza, lakini bado kuna kasoro katika mfumo wa fedha.

Alisema bara la Ulaya linahitaji kushirikiana zaidi kwenye hesabu za bajeti, kulingana na sarafu moja.

Na alisema anataka mfumo wa fedha udhibitiwe zaidi kisheria.

Hapo awali, Rais Obama aliwasihi viongozi wa Ulaya kuweka fedha kwenye mabenki yenye matatizo.