Watakao hujumu amani Somalia watishiwa

Haki miliki ya picha s
Image caption Harakati za kijeshi nchini Somalia

Marekani imetishia kuwekea vikwazo viongozi wa Somalia watakaohujumu mpango wa amani wa umoja wa Mataifa nchini humo

Naibu waziri wa mambo ya nje kuhusu maswala ya Afrika, Johnnie Carson aliyasema hayo baada ya kufanya ziara ya kwanza ya afisaa mkuu yeyote wa Marekani katikam miongo miwili nchini humo.

Alisema ziara yake mjini Mogadishu ilikuwa ni kujionea hatua muhimu ambazo zimepigwa dhidi ya kundi la wapiganaji la al-Shabab.

Hata hivyo wapiganaji hao wenye uhusiano na kundi la al-Qaeda, wangali wanadhibiti sehemu kubwa ya Somalia.

Mwandishi wa BBC Gabriel Gatehouse,ambaye yuko mjini Mogadishu, anasema kuwa mjumbe huyo hakukaa sana mjini humo ingawa alikutana na rais wa Somalia, waziri mkuu na maafisa wengine wa serikali ya mpito.

Lakini bwana Carson alisema kuwa Marekani itamwekea vikwazo yeyote atakaye hujumu mchakato wa kisiasa wa sasa.

"Hatua ambazo tunalazimika kuchukua dhidi ya watakaohujumu mpango huu huenda ni pamoja na kuwanyima visa , vikwazo vya usafiri na hata kupiga tanji mali zao" alisema bwana Carson.

Bwana Carson aliongeza kuwa Marekani inatafakari kuwakeka maafisa wake wa kudumu mjini Mogadishu wakati itakapohisi kuwa kuna usalama wa kutosha.

Pia alipuuza na kutaja kama upumbavu tangazo la Al Shabaab la zawadi ya ngamia kumi kwa yeyote aliye na habari kuhusu maficho ya rais Barack Obama.

Ilikuwa ni jibu la kukejeli tangazo la Marekani wiki jana la zawadi ya dola milioni 3 hadi saba kwa yeyote mwenye habari kuhusu waliko viongozi wa kundi hilo.