Mahakama Misri, kuamua sheria muhimu

Mahakama hiyo inatarajiwa kuamua iwapo sheria iliyopitishwa na bunge, inayowapiga marufuku maafisa waliokuwa katika utawala wa Mubarak kuwania kiti chochote cha umma, ni halali au la, kikatiba.

Iwapo mahakama itaunga mkono sheria hiyo, basi itabidi mgombea urais Ahmed Shafiq, aondolewe katika kinyang'anyiro hicho.

Mahakama ya katiba imetakiwa kutoa uamuzi wake kuhusu iwapo wagombea wawili wa kiti cha urais wanaweza kuwania kiti hicho kikatiba na iwapo uchaguzi wa viti vya ubunge uliofanyika mwaka jana ulikuwa wa halali.

Suala muhimu hapa ni kwa mahakama hiyo kufafanua iwapo sheria inayowazuia watu waliokuwa viongozi wakati wa uongozi wa Hosni Mubarak ni halali.

Iwapo itabainika sheria hiyo ni halali, basi aliyekuwa waziri mkuu Ahmed Shafiq hataweza kushiriki kwenye duru ya pili ya uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa juma hili.

Kwa hiyo, mgombea kiti cha urais wa Muslim Brotherhood, Mohamed Morsi, atakuwa mgombea pekee au uchaguzi huo utarudiwa tena.

Baadhi ya watu hawakutana rais wa taifa hilo kutoka katika chama cha Muslim Brotherhood huku wengine wakisisitiza kuwa watu ambao walihudumu kwenye serikali ya Hosni Mubarak hawapaswi katu kuongoza.

Raia wengine wa nchi hiyo pia wanahofia kwamba huenda nchi hiyo ikarudi tena kwenye machafuko.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC aliyeko Misri, wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanasema kuwa duru ya pili ya uchaguzi itafanyika mwishoni mwa juma ingawaje maamuzi ya mahakama za Misri zimekuwa ngumu kutabiri.