Wagiriki waamua hatima yao

Watu wa Ugiriki wanapiga kura katika uchaguzi wa bunge utakaoamua iwapo taifa hilo litaendelea kuwa miongoni mwa mataifa ya Ulaya yanayotumia sarafu ya euro.

Haki miliki ya picha Reuters

Kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel, ametoa wito kwa raia wa Ugriki kupiga kura ili kuunda serikali itakayoendelea kuunga mkono ubanaji wa matumizi kama njia ya kujikwamua kiuchumi.

Ugiriki imo kwenye uchaguzi muhimu sana ambao matokeo yake ni tabu kutabiri.

Matokeo ya uchaguzi ndio yataamua hatima ya uchumi wa nchi ndogo kabisa kati ya zile zinazotumia sarafu ya euro..na yataamua mustakbali wa sarafu yenyewe.

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameingilia kati kwa kiasi kisichopata kuonekana, wakionya kwamba iwapo Ugiriki itachagua serikali itayokataa kukata matumizi na shuruti za mikopo, basi nchi itafilisika, na pengine itatolewa kwenye mfumo wa sarafu ya euro, na hivo kutapakaza wasiwasi katika nchi nyengine piya za euro.

Chama cha mrengo wa kulia, New Democracy Party, kinaunga mkono sera za kubana matumizi ili kupata mkopo wa Umoja wa Ulaya.

Chama cha mrengo wa kushoto, cha Syriza, kinapinga vikali sera za kukaza mkaja.

Vyama hivo viwli vinavoshindana sasa viko sare kwa mujibu wa kura za maoni.

Kura za maoni zinaonesha Wagiriki wanachukia shida za uchumi, lakini piya wanataka kubaki na euro.

Swala katika uchaguzi wa leo ni jee, wako tayari kujitolea mhanga kwa kiasi gani ili kubaki kwenye euro.