Rwanda yafunga mahakama za gacaca

Serikali ya Rwanda imetangaza kuwa mahakama za kijamii zijulikanazo kama Gacaca zilizoanzishwa ili kuendesha kesi dhidi ya maelfu ya washukiwa wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 zitafungwa rasmi baada ya kumaliza shughuli zake.

Image caption Kesi zilifanywa viwanjani na hata chini ya miti

Mahakama hizo zilianzishwa kama juhudi za kupunguza msongamano katika magereza ya taifa hilo na pia kukuza upatanisho miongoni mwa jamii baada ya mauaji ya kimbari.

Zaidi ya watu 500,000 kutoka jamii za watutsi na wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa katika tukio hilo.

Mkuu wa Idhaa ya maziwa makuu ya BBC Ally Yusuf Mugenzi anasema mahakama hizo zilifufuliwa baada ya kusambaratika kwa idara ya mahakama kufuatia vifo vya mawakili na majaji baada ya vita vya 1994.

Watalaamu wanasema kuwa mwaka wa 2001 kulikuwepo na watuhumiwa 120,000 wa mauaji ya kimbari magerezani na serikali ya Rwanda ilikuwa inatumia dola milioni 20 kila mwaka kuwatunza.

Inakadiriwa kuwa ingechukuwa zaidi ya miaka 100 kuwa hukumu watuhumiwa hao kwenye mahakama za kawaida na zile za jadi zilikuwa fursa bora zaidi kuharakisha kesi hizo.

Mahakama za Gacaca ziliendeshwa na majaji waliochaguliwa na wananchi na walipewa uwezo wa kutoa adabu kali ikiwa ni pamoja ya kuwafunga watuhumiwa maisha jela.

Zaidi ya majaji 250,000 walisikiza kesi hizo katika mahakama hizo zilizofanya vikao vyao hadharani, viwanjani, masokoni na hata chini ya mti.

Hata hivyo mashirika ya kutetea haki za binadamu yalikashifu mahakama hizo kwa kutozingatia vipengee vinavyotambuliwa kisheria za kumpa mstakiwa haki za kujitetea.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 400,000 walifikishwa katika mahakama hizo.

Wanaokosoa mahakama za Gacaca wanasema zilitumiwa na viongozi wa serikali kuzima upinzani.