Morsi akabidhiwa madaraka na Tantawi

Rais wa kwanza wa kiraia wa Misri, na kutoka chama cha Kiislamu, Mohammed Morsi, ameapishwa, na ametoa wito kuwa bunge la nchi lirejeshwe haraka - bunge lilofutwa hivi karibuni.

Katika sherehe kwenye eneo la jeshi nje ya Cairo, kiongozi wa wakuu wa jeshi wanaoongoza nchi, Field Marshal Mohammed Tantawi, alikabidhi madaraka rasmi kwa Rais Morsi.

Hapo awali, akitoa hotuba yake ya kwanza iliyogusia mambo mengi, katika Chuo Kikuu cha Cairo, Bwana Morsi alisema atalilinda jeshi kama taasisi, lakini piya alionya jeshi halifai kuwa mbadala wa matakwa ya wananchi.

Bwana Morsi aliahidi ukurasa mpya utaong'ara katika historia ya nchi, kufwatilia ule aliosema ni ukurasa wa kuchusha.

Alipokuwa akizungumza, akina mama ambao watoto wao waliuliwa chini ya utawala wa Rais Mubarak, walibeba juu picha za watoto wao hao wa kiume.

Bwana Morsi piya alisema Misri haitotapakaza mapinduzi nchi za nje.

Rais mpya aliapishwa kwenye sherehe iliyofanywa katika mahakama ya katiba mjini Cairo.