Mabomu ya arthini yategwa Mali

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mpiganaji wa Kiisilamu Mali

Wapiganaji wa kiisilamu kaskazini mwa Mali wametega mabomu ya arthini mjini Gao baada ya kuudhibiti wiki jana.Wakaazi wa eneo hilo wamesema wapiganaji hao wametega mabomu hayo ili kuzuia mashambulizi ya kundi hasimu la Tuareg.

Makundi yote yalishirikiana katika harakati za kudhibiti kaskazini mwa Mali baada ya kutokea mapinduzi ya kijeshi hapo mwezi Aprili.Wakati huo huo Ufaransa imesema katu haitakubalia magaidi kuweka ngome zao nchini Mali.

Waziri Mkuu wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault ametaja kundi la Al Qaeda Afrika Kaskazini{AQIM} kama tisho kubwa kwa usalama katika kanda kaskazini mwa Afrika na pia kwa Ufaransa.

Matamshi ya Waziri Mkuu yanajiri wakati kundi linaloshirikiana na mtandao wa Al Qaeda Ansar Dine limeharibu misikiti ya kale mjini Timbuktu kwa tuhuma za kujengwa kinyume na Sharia ya Kiisilamu.

Mwendesha mashataka mkuu katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita Fatou Bensouda, amelaani uharibifu huo na kuutaja kama uhalifu wa kivita. Wakaazi katika mji wa Gao wamesema wapiganaji wa kundi la Kiisilamu wametishia maisha yao kwa kuyatega mabomu hayo. Maduka mengi yamefungwa na watu wamesalia manyumbani.

Wapiganaji wa Tuareg ambao wanadaiwa kutaka kuushambulia mji huo wanataka kujitenga na Mali na kuunda eneo huru bila kuzingatia sera za dini. Aidha kundi hili limelaani uharibifu uliotekelezwa na kundi hasimu la Ansar Dine mjini Timbuktu.Msukosuko huu unaoendelea kaskazini mwa Mali umepelekea watu 300,000 kukimbia makaazi yao.