Wahamiaji haramu wakwama baharini

Wahamiaji haramu kutoka Indonesia Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wahamiaji haramu kutoka Indonesia

Meli moja ya jeshi la wanamaji wa Australia imewasili katika eneo ambako meli iliyobeba wahamiaji haramu ipo.

Wakuu wa serikali ya Australia wanasema, hali mbaya ya anga imezuia wahamiaji hao haramu kuabiri meli hiyo ya kijeshi lakini wanamaji hao bado wanadadisi hali ilivyo.

Meli hiyo inasemekana kubeba wahamiaji haramu kati ya 130 na 180, ilitoa ujumbe wa kutaka msaada wa dharura wakati ilipokuwa katika eneo la bahari kati ya Indonesia na Kisiwa cha Christmass.

Tukio hilo limejiri siku moja tu baada ya viongozi wa mataifa hayo mawili, kuahidi kushirikiana katika harakati za kuzuia na kuthibiti ulanguzi wa watu, baada ya meli nyingine mbili iliyokuwa imebeba wahamiaji haramu kuzama mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na shirika linalosimamia na kuthibiti safari za meli nchini Australia, AMSA, meli moja ya mizigo ilikuwa karibu na manuwari hiyo ya kijeshi ilikuwa ikielekea katika eneo hilo.

Manuwari hiyo ya jeshi la wanamaji wa Australia ijulikanayo kama HMAS Wollongong inasemekana kuendlea kuchunguza hali hiyo.

'' kuna ishara za kuthibitisha kuwa meli hiyo ipo hatarini, na hali hiyo itachunguzwa baada ya wanamaji wetu kuabiri meli hiyo na wakati hali ya anga itakapoimarika'' taarifa hiyo ilisema.

Waziri wa mambo ya ndani Jason Clare, amesema meli hiyo ilituma ujumbe wa kutaka msaada wa dharura kwa kuwa lilikuwa inavuja maji.