Kenya lawamani kwa kupuuza Mau Mau

Image caption Mamia ya Mau Mau wamerundikwa kwenye kambi

Mashirika ya kupigania haki za kibinadamu zimeishutumu serikali ya Kenya kwa kukataa kugharimia kesi ambayo wapiganaji wa zamani wa Mau Mau wameishitaki serikali ya Uingereza.

Wapiganaji hao wazamani tayari wamewasili Mjini London kushitaki wakoloni walioitawala Kenya kwa madai ya kuwatesa wakati wakipigania uhuru wa Kenya.

Awali serikali ilitangaza kuwa inaunga mkono kesi hiyo ya Mau Mau.

Lakini wakuu wa serikali wameshindwa kueleza ni kwa sababu gani hawagharimii kesi hiyo.

George Morara alihoji kwanini serikali ya Kenya haitaki kuwasaidi Mau Mau ambao walipigania uhuru wa Kenya wakati serikali hiyo hiyo sasa inawasaidia wakenya mashuhuri ambao wameshitakiwa katika mahakama ya uhalifu wa kimataifa-ICC.

Mwanaharakati huyo amesema kuwa ingawa Mau Mau ilikuwa maarufu katika miaka ya 1950 hadi 60 lakini kuna baadhi ya viongozi wa serikali wanaohofia kuwa kesi hiyo huenda ikawadhuru kisiasa.

Mwandishi wa BBC wa Maswala ya Afrika Martin Plaut anasema imechukua muda mrefu kwa kesi hiyo kufikia hatua ya sasa na huenda ikachukuwa muda mwengine mrefu zaidi kwa Mau Mau kuthibitisha madai ya kuteswa na wakoloni wakati wakipigania uhuru wa Kenya.