Watu 100 wafariki moto Nigeria

Zaidi ya watu mia moja wamefariki na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya lori la mafuta kuanguka kusini mashariki mwa nigeria katika Jimbo la Delta.

Haki miliki ya picha na
Image caption Lori la mafuta

Wakuu wa Serikali wanasema kuwa wenyeji wa eneo hilo walikimbilia kuzoa mafuta yaliokuwa yakichuruzika toka lori hilo lakini likalipuka na na kusababisha maafa hayo.

Mwandishi wa habari Emeka Idika ameiambia BBC kuwa mazishi ya halaiki kwa watu waliofariki kutokana na moto na wasioweza kutambulika yatafanywa katika Jimbo la Rivers wakati wengine wapatao 35 wamelazwa katika hospitali.

Mwandishi huyo ameongezea kusema kuwa idadi ya vifo huenda ikaongezeka kwa sababu kuna baadhi ya watu kutoka vijiji vilivyo karibu na hapo Okogbe waliokua wamekumbwa na balaa la moto mkubwa walikimbilia vichakani na miili yao bado haijaonekana.

Mwandishi mwingine , Oluchi Iwuoha Chimezie, ameiambia BBC kuwa alihesabu zaidi ya maiti 100.

Shirika la habari la Reauters limemnukuu msemaji wa Polisi ya Jimbo la Rivers state, Ben Ugwuegbulam akisema kuwa "mapema leo Lori lililobeba mafuta lilipinduka huko Okogbe na watu kukimbia haraka kujizolea mafuta yaliyokuwa yakimiminika na ghafla bin vuu moto ukalipuka na kusababisha madhara.

Taasisi inayosimamia usalama wa barabarani imesema kuwa Lori hilo liligonga magari matatu. Matukio ya aina hiyo si mageni nchini Nigeria.

Mamiya ya watu wamefariki katika kipindi cha miaka kumi iliyopita wakijaribu kuchota mafuta kutoka mabomba yanayovuja kwa sababu ya kuvunjwa makusudi au watu wanaojaribu kuiba mafuta.

Nigeria ni nchi inayozalisha na kuuza mafuta kwa kiwango kikubwa lakini mamilioni ya raia wake wanaishi maisha ya ufukara.