Marekani yapunguza msada kwa Rwanda

Marekani imekata msaada wa kijeshi inayoipa Rwanda, huku kukiwa na wasiwasi kuwa Rwanda inawasaidia katika mapigano yanayoendelea nchi ya jirani, yaani Jamhuri ya Demokrasi ya Congo.

Haki miliki ya picha AFP

Wizara ya Ulinzi imesema itazuwia dola 200,000 zilizokusudiwa kulisaidia jeshi la Rwanda.

Msaada wenyewe uliokatwa siyo mkubwa kwa jeshi la Rwanda, lakini hatua hiyo inatoa ishara kubwa.

Marekakni inaitetea sana Rwanda katika jumuia ya kimataifa.

Kwa kukata msaada huo, Marekani ni kama inasema "tunaamini ripoti kuwa Rwanda inatibua usalama wa kanda hiyo kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa Congo".

Rwanda imekataa kuwa inawasaidia wapiganaji wa Congo, ambao katika mapigano yao yamepelekea watu laki mbili kuhama makwao.

Mwezi uliopita, Umoja wa Mataifa ulikabidhi ripoti kwa Baraza la Usalama, ambayo ilisema ina ushahidi mzito kuwa Rwanda inalipatia kundi la M23, wapiganaji na zana, na kurahisisha makamanda wao wakubwa kusafiri na kuvuka mpaka baina ya Congo na Rwanda.

Uasi huo ulianza mwezi wa Aprili, wakati wanajeshi mia kadha wa jeshi la Congo walipofanya ghasia.

Uasi huo uliongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye anasakwa na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, kwa uhalifu wa vitani.