Uingereza kuisaidia zaidi Malawi

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Joyce Banda apendeza wahisani

Serikali ya uingereza imeshinikizwa iangalie upya ufadhili wake kwa Malawi baada ya kuwa na uongozi mpya.

Wabunge hao wamesema kwa vile kuna uongozi mpya nchini Malawi hakuna sababu ya kuendelea kuibana nchi hiyo.

Uingereza mwaka 2011 ilisimamisha misaada inayotoa moja kwa moja kwa Malawi na badala yake ilikuwa ikipitisha misaada hiyo kupitia mashirika yasio ya kiserikali.

Hii ni kutokana na madai ya ufisadi na ukiukaji wa haki za kibinadamu.

Lakini sasa kundi la wabunge kutoka Uingereza wanasema kwamba kwa wakati huu nchini Malwai kuna mabadiliko ya kuridhisha tangu Bi Joyce Banda achukue uongozi wa nchi.

Hata hivyo mawaziri wa uingereza wanasema wanataka kuona madadiliko zaidi ya kisiasa na kiuchumi nchini malawi.

Uingereza hutoa Pauni milioni 90 kila mwaka kwa Malawi ambayo ni mojawapo wa nchi maskini zaidi Afrika.

Mingi ya kisaada hiyo inaelekezwa katika sekta ya afya na kilimo.

Lakini misaada ya moja kwa moja ambayo ilikuwa ikipewa serikali katika miradi yake ya kupunguza umaskini ilisimamishwa mwaka 2011.

Hii ni kutokana na madai ya ufisadi na serikali ya Rais wa wakati huyo Bingu wa Mutharika kuwanyanyasa wapinzani wake.

Lakini baada ya kifo cha Mutharika mwezi wa Aprili mwaka huu, uhusiano kati ya Malawi na Uingereza ulianza tena kuimarika.

Wakati huo Waziri wa Maendeleo wa Uingereza Andrew Mitchell alizuru Malawi na kuahidi kwamba nchi yake sasa itasimama na taifa hilo la kusini mwa Afrika.