Rais Mali ataka mazungumzo na Waislamu

Haki miliki ya picha
Image caption Rais wa mpito wa Mali Traore na kiongozi wa mapinduzi Keptein Sanogo

Rais wa mpito wa Mali Dioncounda Traore ametoa wito wa mazungumzo na wapiganaji wa kiislam ambao wanadhibiti eneo la Kaskazini.

Ametoa wito huo wakati akihutubia Taifa kwa mara ya kwanza baada ya kurejea nchini wiki iliyopita kufuatia kutowepo kwa miezi miwili.

Amekuwa kwenye matibabu mjini Paris baada ya kujeruhiwa wakati alipopigwa na wafuasi wa mapinduzi yaliyotokea mwezi Machi.

Waasi wa Tuareg na wapiganaji wa Kiislam waliongeza ghasia zao baada ya mapinduzi na kuchukua udhibiti a eneo la Kaskazini.

Lakini ushirikiano wao umekuwa hauna nguvu na umeanza kuporomoka.

'Wavamizi'

Wapiganaji wa Kiislam sasa wanadhibiti maeneo yote matatu ya miji mikubwa - Timbuktu, Gao na Kidal. Maelfu wamelikimbia eneo la Kaskazini.

Bw Traore alisema ataongoza mazungumzo kuunda serikali ya umoja wa kitaifa nchini Mali na kuongoza juhudi za kuanzisha mazungumzo na Waislamu.

"Wananchi wa Mali hawana budi kuungana dhidi ya wavamizi,” alisema, akimaanisha wapiganaji wa kigeni wa jihadi ambao wanatuhumiwa kudhibiti eneo la kaskazini.

"Kutokana na ugumu wa mgogoro huu na ukubwa wa mateso ya watu wa Kaskazini, kwa pamoja, nasema pamoja, tunaweza kusafisha njia mbele yetu kuiweka huru nchi yetu kutoka kwa wavamizi hawa, ambao wanaacha uharibifu na huzuni, na kuwasababishia watu wetu maumivu, " alisema Bw Traore.

Kumekuwa na shutuma kutoka jumuiya ya kimataifa kwa wapiganaji wa kiislam katika mji wa zamani wa Timbuktu wakilaumiwa kwa kuharibu kumbukumbu za karne nyingi za viongozi muhimu wa dini ya Kiislam ambao wanaheshimika kwa Waislam wa madhehebu ya Sufi.

Imani yao ya Ki-Salafist inapinga kuwaheshimu viongozi waliotukuka wanachukulia makaburi yao kama kuabudu sanamu.

Mr Traore alirejea Mali Ijumaa huku umati wa wafuasi wakiwa wamejipanga barabarani kutoka Uwanja wa ndege mpaka kwenye makazi yake.

Mwandishi wa BBC anasema ingawa kuna matumaini makubwa ya kurejea kwake nchini Mali bado hakuonyeshi pia kama ni ishara ya uwakilishi.