Biashara ya dawa haramu yazidi G. Bissau

Haki miliki ya picha INTERNET
Image caption Wanajeshi wa Guinea Bissau, UN yaonya juu ya dawa za kulevya

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeonyesha wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa biashara ya dawa za kulevya Guinea-Bissau tangu mapinduzi yatokee mwezi April.

Limetaka viongozi nchini humo kurejesha utawaa wa kikatiba.

Guinea-Bissau imekuwa na hisotria ya mapinduzi tangu uhuru wake kutoka kwa Mreno mwaka 1974.

Imekuwa ndio kitovu cha magenge ya kupitishia cocaine kutoka Latin America mpaka Ulaya, ikituhumiwa kushirikiana na maafisa wa jeshi.

"Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wamelaani kitendo cha jeshi kuingilia siasa na kuonyesha wasiwasi wake kuhusu taarifa za kuongezeka kwa usafirishaji wa dawa kuongezeka tangu April 12 mapinduzi yalipotokea." Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilisema katika mkutano wake New York.

Limesema lilikuwa linaangalia uwezekano wa mkutano wa kimataifa kuzungumzia ni kwa namna gani watafanikiwa kurejesha utawala wa kidemokrasia nchini Guinea Bissau.

'Ushawishi'

Mwezi Mei , Baraza hilo liliweka vikwazo vya kusafiri kwa viongozi wa mapinduzi na wanaowaunga mkono.

Jeshi limekubali mazungumzo yasimamiwe na ECOWAS, kurejesha nchi katika utawala wa demokrasia lakini limeshindwa kufanya hivyo.

Mwaka 2010, Marekani iliwashutumu wanajeshi kutoka Guinea-Bissau, wakiwemo mkuu wa jeshi la majini Jose Americo Bubo Na Tchuto, kwa kuhusika na dawa za kulevya.

Katika sheria ya Ushawishi wa Dawa za kulevya , vikwazo vya kifedha viliwekwa.

Hakuna wa kuchaguliwa kwa karibu miaka arobaini sasa ya uhuru ambaye amewahi kumaliza muda wake wa uongozi nchini Guinea-Bissau.