Amnesty yaionya Mali juu ya haki za watu

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais wa mpito wa Mali Dioncunda Traore

Mali inaelekea kutereza kuingia kwenye ‘mgogoro wa haki za binadamu’ Shirika la Kimataifa la Amnesty International limeonya.

Jeshi limekuwa likijihusisha na maamuzi ya mauaji, mateso, na udhalilishaji wa kijinsia tangu mapinduzi ya mwezi Machi, linasema, na kutaka uchunguzi ufanyike.

Jeshi limetoa mamlaka kwa serikali ya mpito lakinibado lina ushawishi mkubwa.

Mali ligawanyika kwenye makundi mawili baada ya mapinduzi huku Kaskazini ikidhibitiwa na wapiganaji wa Kiislam na waasi wa Tuareg.

Wakati huo huo Shirika la Msalaba Mwekundu (ICRC) limezungumza na maafisa wa jeshi 79 wanaoshikiliwa na Vuguvugu la waasi wa Uhuru wa Azawad (MNLA), lilisema.

Ziara hiyo ililenga kuwapatia nafasi wafungwa baada ya miezi ya kukaa kifungoni, mkuu wa ICRC Mali Jean-Nicolas Marti amenukuliwa na shirika la AP likisema.

‘Hatua lazima zichukuliwe kuhakikisha kuwa waliofanya mapinduzi ‘hawaendelei na ukatili wao,’Amnesty International lilisema.

"Tuko wanne. Walitutaka tutoe nguo zetu zote. Tuliambiwa tungiliane kimwili sisi kwa sisi, la sivyo wangetuua wote," Afisa mmoja amenukuliwa akisema na shirika la Amnesty.

Takriban askari 21 hawajulikani waliko tangu kwa kujaribu kupinga mapinduzi hayo mwezi April, Amnesty lilisema.

Limeongeza kuwa wafungwa wanalazimishwa kukiri makosa baada ya kuteswa mikono yao ikiwa imefungwa nguo zao zimesokomezwa midomoni na sigara zikizimwa masikioni mwao.

"Vitendo hivi vya kikatili vinapita sheria za Haki za Biandamu Mali na hatua lazima zichukuliwe ili wanaofanya ivtendo hivi wasiendelee’Amnesty lilisema.

Jeshi lilifanya mapinduzi baada ya serikali ya kuituhumu kushindwa kumaliza uasi kaskazini.

Lakini waasi wa Tuareg na wapiganaji wa Kiislam walitumia fursa hiyo ya mapinduzi na kushika maeneo makubwa ya kaskazini.

Wapiganaji wa Kiislam wameharibu hifadhi za kale za mji wa Timbuktu na kudharau maonyo ya Umoja wa Mataifa na makudni mengine kuwa walikuwa wakifanya uhalifu.