‘Mgogoro wa chakula ni wa kudumu Sahel’

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Njaa Sahel inaripotiwa kuwa ya kudumu

Zaidi ya watoto milioni moja wako katika hatari ya kupata utapiamlo katika ukanda wa Sahel Afrika Magharibi kwa mujibu wa wa mashirika mawili ya kiraia.

Shirika la World Vision na Save the Children yanasema mamilioni ya familia wanahangaika kwa kile kinachoelezwa kuwa ni athari kubwa ya ukosefu wa chakula.

Wanasema sababu kubwa ni ukame au upungufu wa chakula, lakini pia hakuna uhakika wa chakula kutokana na bei kubwa ya chakula.

Mashirika hayo yanataka uwekezaji zaidi kwenye chakula.

Hata inapokuwa ni mwaka wa kawaida vifo 200,000 vya watoto vinawza kuhusishwa moja kwa moja na utapiamlo,’ walisema.

Ukanda wa Sahel ni eneo kame linalojumuisha pia Mauritania, Mali, Niger, Burkina Faso, Senegal na Chad.

Zaidi ya watu milioni 18 katika eneo hilo kwa sasa wamekubwa na njaa, mashirika hayo yamesema.

Mkurugenzi wa masuala wa dharura wa World Vision Paul Sitnam alisema: "Watu maskini kabisa …kimsingi hawawezi kupta chakula chochote sokoni kwa sababu ya ufukara wa muda."

Alisema tatizo haliwezi kutatuliwa kwa kugawa tu chakula, na jumuiya ya kimataifa inahitaji kupeleka msaada wa haraka katika maeneo yaliyoathiriwa kuweka urahisi w wa kukabiliana na ‘mtikisiko’ huo.

"Kuhakikisha pia kuwa kuna muungano wa kifamilia, miundo mbinu na usalama wa kijamii kutoa uangalizi kwa watoto na familia zao wakati wa mgogoro kama huu " alisema.

Upungufu wa mazao, kupanda kwa bei za mazao na uhaba wa chakula katika nchi jirani kunachangia kuwa na tatizo sugu, Save The Children linasema.

Mwezi Januari, Oxfam na Save the Children yalisema maelfu ya watu katika Pembe ya Afrika walikufa kwa njaa mwaka jana kwa sababu jumuiya ya kimataifa ilishindwa kutoa onyo mapema.

Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Justin Forsyth, anatoa wito wa kujadili hili katika "mkutano wa njaa", unaotarajiwa kufanyika baada ya michezo ya Olympic London.

Viongozi wa Dunia, wafanyabiashara wakubwa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wanaharakati wa maendeleo watahudhuria mazungumzo katika siku ya mwisho ya michezo.