Shambulio la mpakani laipa Israel kiwewe

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mpaka kati ya Misri na Israel katika eneo la Sinai

Rais wa Misri , Mohammed Mursi, ameahidi kuwa vikosi vya usalama vya Misri, vitachukua uthibiti kamili wa rasi ya Sinai baada ya shambulio lililotokea kwenye mpaka baina ya nchi hiyo na Israel.

Watu waliojihami kwa silaha waliwauwa walinzi sita wa mpaka wa Misri.

Israel ilisema washambuliaji waliokuwa wamejihami kwa silaha nzito walichukua magari ya kijeshi na kujaribu kulazimisha kuvuika mpaka huo .

Shambulio hilo lilitokea jioni katika kizuizi cha mpakani wakati wanajeshi walikuwa wakifunga kazi tayari kwa futari wakati huu wa mfungo wa mwezi wa Ramadhan.

Televisheni inayomilikiwa na serikali nchini Misri imesema kuwa kundi la watu waliojihami kwa mbuduki na maguruneti ya kurushwa kwa roketi liliwashambulia wanajeshi hao kabla ya kutoweka na gari moja la kivita.

Msemaji wa jeshi la Israel, hata hivyo alisema magari mawili yalitekwa na kwamba moja lililipuka karibu na eneo la kivuko cha mpakani la Kerem.

Gari la pili lililengwa na jeshi la wanahewa la Israel.

Tukio hilo litachukuliwa kama ushahidi wa kutia wasiwasi kwamba wanamgambo wa Kiislamu wanathibiti eneo la kaskazini mwa Jangwa la Sinai.

Wanamgambo hao wamelaumiwa kurusha maroketi kadhaa nchini Israel na kuwauwa Waisraeli tisa mwaka uliopita.

Wakati hali ya wasiwasi ikizidi kutanda Misri imetuma vifaru zaidi na wanajeshi katika eneo la Sinai-Mpango huo ulitekelezwa kwa makubaliano na Israel katika mkataba wa amani wa mwaka 1979.

Israel imeitaka Misri kuchukuwa uamuzi wa mara moja.

Tukio hilo limejiri wakati Israel ikitangaza kuwa inaboresha makombora yake ya masafa marefu aina ya Ballistic kukabiliana na kile inachokiona kuwa tishio la usalama wake linalozidi kujitokeza katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mradi huo wa kujenga makombora ya masafa marefu unatekelezwa na serikali ya Israel kwa ushirikiano na Marekani.

Hii ni baada ya Iran kutangaza kuwa imefanikiwa katika kufanyia majaribio makombora yake ya masafa mafupi aina ya Ballistic, yaliyoboreshwa zaidi.