Picha zaonyesha maangamizi Syria

Imebadilishwa: 8 Agosti, 2012 - Saa 03:47 GMT

Waasi katika mji wa Aleppo.

Shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, linasema picha mpya za satellite zinaonyesha ni kwa kiwango kipi silaha nzito zilitumiwa kutekeleza maangamizi katika maeneo ya mji wa Aleppo nchini Syria.

Shirika hilo limeionya serikali na vikosi vya waasi kuwa huenda vikakabiliwa na mashtaka ya uhalifu kwa kushindwa kuwalinda raia .

Shirika la Amnesty International linasema kuwa picha hizo za Satelite zinaibua maswala ya dharura kuhusu shambulio la hivi punde katika mji uliozingirwa kijeshi wa Aleppo - picha hizo zinaonyesha ongezeko katika matumizi ya silaha nzito nzito karibu na maeneo ya makaazi ya raia.

Amnesty inasema baadhi ya picha hizo zinaonyesha zaidi ya mashimo makubwa mia sita ambayo huenda yamesababishwa na milipuko ya mizinga wakati wa mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali na makundi ya upinzani katika mji wa Anadan karibu na Aleppo.

Baadhi ya wataalamu wasioegemea upande wowote ambao wamezungumza na BBC wamekubaliana na ufafanuzi wa shirika la Amnesty kuhusu picha hizo.

Aliyekuwa waziri wa maswala ya mashariki katika serikali ya chama cha Leba nchini Uingereza, Kim Howells, amesema kuwa Syria bado itashuhudia umwakigaji wa damu kwa miezi kadhaa ijayo kabla ya kupatikana suluhu ya mgogoro huo.

Hatua ya kuugeuza mji mkubwa zaidi nchini Syria na kuwa ulingo wa vita, shirika la Amnesty linaonya, itazua maafa ya raia wengi. Shirika hilo linasema ujumbe wake kwa pande zote mbili zinazopigana ni kwamba, 'mashambulizi yoyote dhidi ya raia yataratibiwa bayana'' ili wale wanaohusika wapate kuwajibika baadaye.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.