Brazil yapokea bendera ya Olimpiki 2016

Kufunga Olimpiki Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bendera za mataifa washiriki wa Olimpiki zapeperushwa katika sherehe za kufunga mashindano hayo mjini London.

Bendera rasmi ya Olimpiki imekabidhiwa kwa Brazil, ambapo mji wa Rio de Janeiro utakabiliwa na jukumu la kuandaa michezo hiyo mwaka wa 2016.

Maonyesho ya kufunga olimpiki ya Londono 2012 yalikuwa na mbwembwe.

Maelfu ya mashabiki walikusanyika kuaga michezo hiyo na kutumbuizwa na wasanii maarufu zaidi duniani akiwemo George Michael, Spice girls, muziki ya wababe kama vile Beatles na Queen vile vile ilipamba tamasha hizo.

Rais wa kamati ya kimataifa ya michezo ya Olimpiki Jacque Rogge alitaja michezo hiyo ya mjini London kuwa ya kufana na kutumbuiza.

Hata hivyo matokeo ya Afrika Mashariki, ndiyo yaliyoyokashifiwa pakubwa zaidi. Hasa nchi kama vile Kenya na Ethiopia. Wengi wanaona kuwa wababe hao waliotazamiwa kuchukua nafasi za mwanzo za dhahabu katika mbio za masafa mbali mbali, walishindwa kushikilia rekodi zao na hata kupata pigo kutoka kwa wakimbiaji wapya.

Akizungumza na BBC mjini London, mhariri wa michezo wa gazeti moja la Kenya, Elias Makori, amesema kuwa Kenya ilizorota katika riadha kutokana na uzembe wa usimamizi wa michezo. Alisema hali hiyo iliwavunja mioyo wanaspoti na akapendekeza kuwa maafisa wote wanaosimamia shughuli za riadha nchini Kenya waachishwe kazi.

Mbio za mwisho mwisho zilikuwa za kuchangamsha zaidi huku zikiwashtua mashabiki kwa kutokea chipukizi kama vile Uganda katika medani ya Dhahabu ikiwa ni mara ya kwanza kabisa katika miaka zaidi ya arobaini kwa nchi hiyo.

Mwandishi wa BBC wa Uganda, Isaac Mumena, alisema wananchi wamefurahia ushindi wa Stephene Kiprotich katika marathon. Kiprotich ni nyota mkuu wa taifa hilo baada ya kumaliza ukame wa medali ya dhahari kwa zaidi ya miaka kumi kwa taifa lake la Uganda.