Oscar Pistorius aomba radhi kwa matamshi yake

Imebadilishwa: 3 Septemba, 2012 - Saa 10:07 GMT

Pistorius na Olivera

Mwanariadha mlemavu wa Afrika Kusini Oscar Pistorius, ameomba radhi kwa matamshi yake baada ya kushindwa katika fainali za mita miambili kwenye michezo ya olimpiki ya walemavu inayoendelea mjini London.

Pistorius kutoka Afrika Kusini aliishutumu kamati ya kimataifa ya olimpiki ya walemavu na kusema kuwa mshindani wake aliyemshinda kwenye mbio hizo alikuwa na miguu bandia mirefu kuliko yake.

Pistorius aliongeza kuwa anahisi swala hilo bado linastahili kuchunguzwa kwa kina.

Alinukuliwa akisema '' Nataka kuomba radhi kwa matamshi yangu ingawa nahisi kama bado swala hili linapaswa kuchunguzwa zaidi.''

Bingwa huyo wa dunia alishindwa na mshindani wake kutoka Brazil, Alan Oliveira katika fainali za mbio za mita miambili.

Awali kamati ya kimataifa ya michezo ya olimpiki ya walemavu ilipuuzilia mbali malalamishi yaliyotolewa na mwanariadha huyo kuhusu vyuma vya miguuni vya mshindani wake Alan Oliveira.

"nakubali kuwa kutoa malalamishi yangu punde tu baada ya mashindano lilikuwa kosa kubwa'' aliongeza Pistorius

"huo ulikuwa ushindi wa Alan na ningeta watu wafahamu kuwa namuheshimu sana.''

Najivunia kushiriki katika olimpiki ya walemavu na ninaamini lazima pawepo usawa kwenya michezo''.

Pistorius alikuwa amesema kwamba hapakuwa na usawa katika fainali ya shindano la mbio za mita mia mbili katika michezo hiyo inayoendelea ambayo alishindwa.

Akizungumza baada ya kumaliza wa pili nyuma ya mwanariadha Alan Oliveira kutoka Brazil, Pistorius alinung'unika kuwa vyuma vya kukimbilia alivyokuwa anatumia mshindani wake vilikuwa virefu kuliko vyake.

Hata hivyo kamati hiyo imesema kuwa vyuma vya Olivera vilikuwa vimepimwa na hakuna sheria zilizovunjwa.

Alan Olivera kwa upande wake amesema anaamini Pistorius hafahamu ukweli na kwamba vyuma vyake vilikwishakaguliwa na maafisa wa michezo kabla ya shindano.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.