Brahimi ashutumu dunia kwa kupuuza Syria

Imebadilishwa: 3 Septemba, 2012 - Saa 04:50 GMT

Lakhadar Brahimi, Mwakilishi wa UN nchini Syria

Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa juu ya Maswala ya Syria, Lakhadar Brahimi, amesema jamii ya kimataifa haifanyi cho chote kikubwa kusimamisha mauaji nchini Syria.

Mtangulizi wa Bwana Brahimi, Kofi Annan, alijiuzulu Agosti baada ya mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na waasi kuongezeka nchini humo, huku pande zote mbili zikipuuza mapendekezo yake.

Kwingineko Serikali ya Jordan imeongeza maradufu kiwango cha pesa inachosema inahitaji kutoka jamii ya kimataifa kukabiliana na idadi kubwa ya wakimbizi wanaoingia nchini humo kutoka Syria.

Katika wito iliyotoa kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia wakimbizi, Jordan ilisema inahitaji kwa upesi dola Milioni 700. Waziri wa Mipango, Jafaar Hassan, alisema anatazamia idadi ya Wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya usalama nchini humo kupanda hadi robo milioni.

Wakati huo huo, Serikali ya Syria imesema kuwa wanajeshi walio waaminifu kwa Rais Assad wamelitimua kundi kubwa la waasi waliokuwa wamevamia chuo cha wanahewa karibu na jiji la Aleppo.

Ingawaje kituo cha Televisheni kimeripoti ushindi wa serikali katima maeneo kadhaa, waandishi wa habari wamesema kuwa Serikali haina dalili yo yote ya kuukomboa Aleppo au kusimamia vitongoji vyote vya jiji la Damascus.

Umoja wa Mataifa unataka Serikali ya Syria kuondoa silaha zake kubwa kubwa kutoka miji nchini humo kama hatua ya kutoa mazingira ya kuanzisha mashauriano kati ya pande hizo mbili zinazozozana.

Akiwahutubia wanafunzi katika taasisi ya mashauri ya Kigeni, waziri wa mashauri ya Kigeni wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema nchi yake inataka amani nchini Syria.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.