Migomo ya wachimba migodi yasambaa Afrika Kusini

Imebadilishwa: 12 Septemba, 2012 - Saa 15:37 GMT

Migomo ilienea katika sekta ya uchimbaji migodi kote Afrika Kusini hii leo. Kazi katika migodi inayomilikiwa na kampuni ya madini ya dhahabu nyeupe, Anglo-American imeakhirishwa.

Kampuni hiyo imesema kuwa imepokea vitisho kutoka kwa waandamanaji katika mgodi huo.

Wachimba migodi katika mgodi wa dhahabu walitawanyishwa kwa kurushiwa mabomu ya kutoa machozi.

Maelfu ya watu walionekana wakitoroka kutoka eneo hilo la tukio, huku wakinawa nyuso zao kwa maji ya mto uliokuwa karibu kutuliza machungu ya gesi hiyo ya kutoa machozi.

Mapema leo mwanaharakati wa kisiasa nchini Afrika Kusini Julius Malema alitoa wito wa maandamano makubwa ya kitaifa nchini humo kwa wafanyakazi wa migodini.

"wamekuwa wakiiba madini haya ya dhahabu kutoka kwenu." bwana Malema aliwaambia wachimba migodi waliokuwa wanamshangilia katika mgodi mmoja wa dhahabu mashariki mwa Johannesburg.

"sasa ni wakati wenu." aliongeza Malema.

Migomo ya wachimba migodi imekumba Afrika Kusini na kuathri shughuli za kuchimba madini ya Platinum na dhahabu katika nchi hiyo yenye rasilimali nyingi.

Lakini baadhi wanamtuhumu Malema kwa kuwa na njama na kujinufaisha kisiasa huku wengi wakiwa bado wanaomboleza vifo vya wachimba migodi 34 wa Marikana mwezi jana nchini humo.

Watu 44 walifariki katika mgodi huo katikati ya mwezi Agosti. 34 wakipigwa risasi na kuuawa na polisi kwa siku moja.

Tume ilibuniwa na serikali kuchunguza matukio katika mgodi huo.

Wadadisi wanasema kuwa kuangazia baadhi ya mambo yanayohusu chama cha ANC kama uhusiano wake na biashara kubwa kubwa pamoja na kupuuza wananchi wafanyakazi ambao wamekuwa daima wakiunga mkono chama hicho bila shaka ni mwiba kwa chama tawala.

"lazima mgomo wa kitaifa ufanyike," Malema aliwaambia wafanyakazi wanaogoma katika machimbo ya dahahabu ya KDC.

''Yametosha! Tumesubiri miaka mingi kunufaika na madini haya. Lazima sasa mfaidike na nyiyi kutokana na dhahabu hii.'' alisema Malema.

Wakati akitoa hotuba yake, Malema alishangiliwa sana watu wakipiga firimbi na mbinja pamoja na kupuliza vuvuzela.

Malema alifurushwa kutoka chama tawala ANC na angali anachunguzwa kwa madai ya ufisadi . Lakini anaendelea kuzua hisia miongoni mwa umma hasa kufuatia mauaji ya wachimba migodi mwezi jana.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.