Rais wa Somalia anusurika kifo

Imebadilishwa: 13 Septemba, 2012 - Saa 09:30 GMT

Rais Sheikh Mohamud na Waziri Sam Ongeri wa Kenya

Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud , amenusurika jaribio la kumuua mjini Mogadishu.

Milipuko miwili ilitokea nje ya lango la makao yake katika hoteli ya Al-Jazeera wakati rais huyo alipokuwa anafanya mkutano na waandishi wa habari.

Mwandishi wa BBC mjini Mogadishu alisema kuwa watu saba wakiwemo wawili waliofanya shambulizi hilo la kigaidi dhidi ya hoteli alimokuwa rais mpya Hassan Sheikh Mohamud waliuawa.

Kundi la wanamgambo la al-Shabaab limekiri kufanya shambuliizi hilo.

Mnamo siku ya Jumanne kundi hilo lilisema kuwa uchaguzi wa rais mpya ambayo ndiyo hatua ya hivi karibuni kujaribu kumaliza vita vya Somalia, ulipangwa na maadui wa Somalia.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa miaka mingi rais wa Somalia kachaguliwa nchini humo.

"hili shambulizi la kinyama linakuja siku mbili tu baada ya hatua kubwa ambapo wabunge wa Somalia walimchagua rais Hassan Sheikh Mohamud na kuwapa watu wa Somalia matumaini mapya ya mustakabali mzuri,'' alisema mjumbe maalum wa umoja wa mataifa kuhusu Somalia Augustine Mahiga.

''Jitihada kama hizi za kurejesha nchi katika machafuko hazitazuia ari ya watu wa Somalia kutaka kupiga hatua,'' aliongeza bwana Mahiga

Shambulizi hilo lilifanyika wakati rais Mohamud akifanya mkutano na waandishi wa habari na waziri wa mambo ya nje wa Kenya Sam Ongeri aliyeongoza ujumbe wa Kenya kwenda kumpongeza rais mpya wa Somalia.

Mtu mmoja aliyeshuhudia tukio hilo aliambia BBC kuwa watu wawili waliegesha gari lao karibu na hoteli hiyo na kisha kutembea hadi jengo hilo liliko.

Mmoja alijilipua karibu na lango la hoteli hiyo wakati wa pili akiingia ndani ya hoteli hiyo na kufyatua bunduki na kumjeruhi mlinzi mmoja.

Mtu wa pili alipigwa risasi na kuuawa kabla ya kujilipua.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.