Magharibi: komesheni maandamano

Imebadilishwa: 15 Septemba, 2012 - Saa 16:34 GMT
Waandamanaji walipowasha moto katika ubalozi wa Marekani mjini Tunis, Tunisia

Waandamanaji walipowasha moto mkubwa katika ubalozi wa Marekani mjini Tunis, Tunisia

Mataifa ya nchi za magharibi yametaka kukomeshwa kwa maandamano yenye lengo ya kushambulia balozi za nchi hizo kupinga filamu inayomdhalilisha mtume Muhammad iliyotengenezwa nchini Marekani.

Jumuiya ya Ulaya imewataka viongozi wa nchi za Kiarabu na nchi nyingine za kiislamu kuacha maandamano na kudumisha amani.

Marekani inatuma wanajeshi wake kulinda ubalozi wake ulioko Khartoum nchini Sudan ikiiasa pia Sudan kulinda balozi za kigeni nchini humo.

Watu wasiopungua saba waliuawa katika maandamano ya ghasia mjini Khartoum, Tunis na Cairo siku ya Ijumaa, na kuna wasiwasi wa kutokea maandamano zaidi.

Wanajeshi wa Marekani walipelekwa pia nchini Libya siku ya Jumatano baada ya balozi wa Marekani nchini Libya na Wamarekani wengine watatu kuuawa pia nchini Yemen siku ya Ijumaa baada ya ghasia za maandamano mjini Sanaa.

Nchini Afghanistan, wapiganaji wa Taliban wamesema pia wameshambulia moja ya kambi kubwa za vikosi vya kimataifa nchini humo ya Bastion ambapo wanajeshi wawili wa Marekani waliuawa.

Wapiganaji hao wanadai kufanya shambulio hilo kulipiza kisasi kupinga filamu hiyo ya kuukashifu uislamu.

Waandamanaji wakipinga filamu hiyo mjini Sydney Australia siku ya Jumamosi, 15 Septemba 2012

Waandamanaji wakipinga filamu hiyo mjini Sydney Australia siku ya Jumamosi, 15 Septemba 2012

Balozi za Ujerumani na Uingereza nchini Sudan pia zilishambuliwa ingawaje uhusiano juu ya filamu hiyo na nchi hizo haujafahamika.

Siku ya Ijumaa rais wa Marekani Barack Obama na Waziri wa mambo ya nchi za nje Hillary Clinton walihudhuria mapokezi ya kurejeshwa Wamarekani waliouawa mjini Benghazi nchini Libya.

Bwana Obama alisema kuwa Marekani itakabiliana vilivyo dhidi ya mashambulizi yoyote kwa balozi zake nchi za nje.

Maandamano zaidi yameripotiwa kuenea zaidi hadi nchini Australia ambapo polisi walipambana na mamia ya waislamu katika mitaa ya jiji la Sydney.

Polisi hao walitumia gesi ya kutoa machozi na mbwa kujaribu kuwasambaratisha waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe na miti.

Mtengenezaji ahojiwa

Wakati huohuo mmoja wa watu wanaoshukiwa kuhusika na utengenezaji wa filamu hiyo inayolalamikiwa kuukashifu Uislamu, amehojiwa na maafisa wa polisi mjini Los Angels nchini Marekani.

Wanataka kujua iwapo alikiuka masharti ya msamaha wa parole aliokuwa amepewa kufuatia adhabu ya kifungo kwa makosa ya kughushi.

Aliadhibiwa adhabu ya kifungo jela mwaka 2010 kwa kughushi kujipatia fedha benki na baadaye alipewa msamaha wa masharti.

Adhabu hiyo pia ilimpiga marufuku kutumia vifaa vya kompyuta na intaneti.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.