Ulaya yasitisha msaada kwa Rwanda

Imebadilishwa: 25 Septemba, 2012 - Saa 16:38 GMT

Waasi wa M23

Muungano wa Ulaya umeamua kusitisha msaada kwa Rwanda.

Uamuzi wa Muungano huo umefikiwa kufuatia ripoti ya baraza la usalama la Umoja huo iliyodai kwamba Rwanda inaunga mkono waasi wa M23 dhidi ya serikali ya Congo.

Waasi hao wanadhibiti kimabavu sehemu kubwa ya Mashariki mwa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo na hata kuwatoza kodi wananchi.

Kundi hilo lilianza uasi katika eneo hilo mwezi Aprili na kusababisha takriban watu nusu milioni kukimbilia usalama wao.

Lakini Rwanda imeendelea kukana madai hayo.

Umoja wa Mataifa unafanya mkutano na baadhi ya yatakayopewa kipaombele kwenye mkutano huo ni swala la mgogoro huo Mashariki mwa Congo.

Mapema mwezi Julai Marekani ilizuia dola 200,000 zilizokusudiwa kulisaidia jeshi la Rwanda.

Msaada wenyewe uliokatwa siyo mkubwa kwa jeshi la Rwanda, lakini hatua hiyo ilitoa ishara kubwa.

Kwa kukata msaada huo, Marekani ni kama ilikuwa inasema "tunaamini ripoti kuwa Rwanda inatibua usalama wa kanda hiyo kwa kuwaunga mkono wapiganaji wa Congo".

Mwezi Juni ,Umoja wa Mataifa ulikabidhi ripoti kwa Baraza la Usalama, ambayo ilisema ina ushahidi mzito kuwa Rwanda inalipatia kundi la M23, wapiganaji na zana, na kurahisisha makamanda wao wakubwa kusafiri na kuvuka mpaka baina ya Congo na Rwanda.

Wanawake Mashariki mwa Congo wakilaani maasi

Uasi huo ulianza mwezi wa Aprili, wakati wanajeshi mia kadha wa jeshi la Congo walipofanya ghasia.

Uasi huo uliongozwa na Jenerali Bosco Ntaganda, ambaye anasakwa na Mahakama ya Jinai ya Kimataifa, ICC, kwa uhalifu wa kivita.

Nayo serikali ya Uholanzi ilisitisha msaada wa dola milioni 6.15 kwa Rwanda baada ya nchi hiyo kuhusishwa na madai hayo ingawa baadaye ilianza tena kutoa msaada kwa nchi hiyo baada ya serikali ya Rwanda kuahidi kushirikiana na kukomesha vita hivyo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.