Jeshi la Kenya lashambulia maslahi ya Al Shabaab

Imebadilishwa: 27 Septemba, 2012 - Saa 13:06 GMT

Jeshi la Kenya

Jeshi la Kenya linasema kuwa ndege zake za kivita zimeshambulia uwanja wa ndege mjini Kismayo na kuharibu ghala yenye silaha za wanamgambo wa Al Shabaab.

Mji wa Kismayo Kusini mwa Somalia ndio ngome kubwa ya kundi hilo ambalo lina uhusiano na Al Qaeda.

Msemaji wa al-Shabab amesema kuwa hakuna aliyejeruhiwa wala kuuawa katika mashambulizi hayo na kwamba hapakuwa na uharibifu wowote wa mali.

Wanajeshi wa Kenya wanashirikiana na wale wa Muungano wa Afrika kupambana vikali na wapiganaji wa Al Shabaab ambao wamesababisha msukosuko nchini Somalia kwa muda mrefu.

Al-Shabab wamelazimika kuondoka kutoka mji mkuu,Mogadishu, na katika miji mingine kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita ingawa bado wanadhibiti sehemu kubwa ya Kusini na maeneo ya kati mwa Somalia.

Takriban watu 10,000 wameutoroka mji wa Kismayo katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR idadi kubwa ya watu wameuotoroka mji wa Kismayo huku makabiliano yakipamba moto.

Kenya ilianza harakati zake nchini Somalia mwaka mmoja uliopita, baada ya kukithiri kwa mashambulizi kwenye mpaka wake na Somalia ambayo Al Shabaab ililaumiwa kuyatekeleza.

Mapema wiki hii Rais wa Kenya Mwai Kibaki, aliambia mkutano wa baraza kuu la Umoja wa Mataifa kuwa, anatumai wakimbizi wa Somalia wanaoishi Kenya wataweza kupelekwa katika kile alichokiita maeneo huru ya Somalia.

Kenya inahifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wa kisomali katika kambi ya Dadaab waliokimbia vita na njaa nchini Somalia katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.