Ushindani mkali dhidi ya Hugo Chavez

Imebadilishwa: 1 Oktoba, 2012 - Saa 08:56 GMT

Wafuasi wa kiongozi wa upinzani katika mkutano wa hadhara mjini Caracas

Kiongozi wa upinzani nchini Venezuela Henrique Capriles amevutia umati mkubwa wa wafuasi katika kampeini yake ya mwisho ya uchaguzi mkuu mjini Caracas.

Bwana Capriles , alimkosoa Rais Hugo Chavez kwa kile alichokiita orodha ndefu ya ahadi ambazo hajawahi kutimiza.

Aidha alidai haki kwa wanaharakati watatu wa upinzani waliouawa wakati wa maandamano katika jimbo la Barinas siku ya Jumamosi.

Bwana Capriles alihutubia umati mkubwa wa wafuasi wake katika jimbo la Zulia akiahidi kuendeleza mfumo wa ujamaa ikiwa atachaguliwa kwenye uchaguzi utakaofanyika tarehe 7 mwezi huu.

Melfu ya watu walifurika kwenye barabara za mji mkuu Caracas siku ya Jumapili, kumuunga mkono bwana Capriles.

"nadhani huu ni mkutano mkubwa wa hadhara kuwahi kushuhudiwa mjini Caracas " alisema bwana Capriles.

Bwana Chavez pia aliwavutia maelfu ya wafuasi katika jimbo la Zulia. Ghasia zilikumba kampeini hizo cha uchaguzi mkuu huku kukitokea vifo vya watu watatu siku ya Jumamosi.

Rais Chavez amewatahadharisha wananchi kuwa ikiwa upinzani utashinda uchaguzi huo , nchi hiyo huenda ikarejea nyuma miaka 30.

"Mimi sijawadanganya wala sijakosa kuwatimizia mahitaji yenyu," alisema rais Chavez.

Kumekuwa na visa vingine vya vurugu na ghasia wakati huu wa kempeini za uchaguzi. Wafuasi wa pande zote mbili walirushiana mawe mapema mwezi Agosti, wakati bwana Capriles alipojaribu kupita katika mji wa Puerto Cabello.

Huku wasiwasi mkubwa kwa wapiga kura ukiwa uhalifu sugu, mwandishi wa BBC Sarah Grainger, anasema kuna hofu ghasia zaidi huenda zikalipuka katika kile kinachosemekana kuwa uchaguzi ambao umekuwa na ushindani mkali sana .

Bwana Chavez amekuwa mamlakani tangu mwaka 1999, na aligundulika kuwa na saratani mwaka jana.

Zaidi ya vyama thelathini vya upinzani, vimemuunga mkono bwana Capriles.

Nini maoni yako kuhusu uchaguzi mkuu nchini Venezuela? Je unahisi rais Chavez ametawala vya kutosha?

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.