Msako mkali baada ya mauaji Nigeria

Imebadilishwa: 3 Oktoba, 2012 - Saa 12:41 GMT
Chuo kikuu cha Mubi, Nigeria

Maafisa wa usalama nchini Nigeria wanafanya msako wa nyumba hadi nyumba kufuatia mauaji ya halaiki katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Polisi wanasema ni watu 25 waliofariki lakini idadi kamili ya waliouawa bado haijabainika.

Matukio yanayohusishwa na kundi la wapiganaji la Boko Haram yameripotiwa katika mji wa Mubi.

Hata hivyo, Serikali inashuku uhasama wa kisiasa miongoni mwa wanafunzi huenda ulichochea mauaji hayo.

Msemaji wa Jimbo la Adamawa amekiri kwamba Polisi bado hawajapata muelekeo wa kutosha kuendeleza uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo.

Hata hivyo, amesema uhasama wa kisiasa miongoni mwa wanafunzi huenda umechangia pakubwa.

Uchaguzi wa Wanafunzi ulifanyika katika chuoni hicho cha mafunzo anuwai Mjini Mubi mwishoni mwa juma lililopita.

Baadaye Jumatatu iliyofuatia, kundi la wanaume lilitekeleza kile kilichoonekana kuwa mauaji yaliyowalenga watu fulani.

Picha za kuogofya zilionyesha maiti za vijana kadha, nguo zao zikiwa zimetapakaa damu huku vipaji vya uso vikiwa na majeraha makubwa.

Kuna historia ya mauaji katika matawi ya vyuo vikuu nchini Nigeria ambapo hali inakuwa mbaya zaidi pale magenge ya wanafunzi yanapokabiliana na Polisi, lakini hali bado haijafikia kiwango cha mauaji ya Mubi.

Mapema mwaka huu, visa vinavyohusishwa na wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram vimeripotiwa mjini humo ambapo wanajeshi waliwatia nguvuni washukiwa kadha, suala linalopelekea Boko Haram kushukiwa kuhusika na mauaji hayo.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.