Mafuriko yaibua wanyama hatari, Nigeria

Imebadilishwa: 4 Oktoba, 2012 - Saa 09:04 GMT
Mafuriko nchini Nigeria

Wanyama hatari kama vile Mamba, Nyoka na Viboko wameanza kuingia kwenye makaazi ya watu katika eneo la kati nchini Nigeria.

Mafuriko makubwa yaliyokumba Nigeria yamepelekea mito iliyofurika kusomba wanyama hao hadi kwenye nyumba za wenyeji.

"kuna kiboko ndani ya nyumba yangu," Mkaazi wa Jimbo la Benue Wuese Jirake akaiambia BBC. "natarajia kiboko huyo ataondoka atakapochoka kujificha nyumbani kwangu."

Mamia ya watu wamefariki na wengine kuachwa bila makao huku mashamba yakiharibiwa na mafuriko hayo makubwa zaidi kuwahi kukumba Nigeria kwa miongo mingi.

'tunatumai yatakwisha' Jirake akaiambia BBC akiongezea kwamba kwa hivi sasa maji yamejaa nyumbani kwake kufikia kina cha kiunoni.

"iwapo kuna njia ya kumuondoa kiboko huyu basi maafisa wa Serikali wanafaa kunisaidia."

Kulingana na Mwandishi wa BBC Is'haq Khalid, hali kama hiyo pia imeripotiwa katika Miji ya Makurdi, Agatu, Logo na Adoka.

Shirika la taifa la kushughulikia hali za dharura limesema linashirikiana na Wakuu wa Jimbo la Benue na wahusika wengine kuhakikisha walioathirika na mafuriko wamerudi kwenye nyumba zao.

Mshirikishi wa Shirika hilo katika eneo la kaskazini ya kati nchini Nigeria, Abdussalam Muhammad, ameiambia BBC kwamba sio salama kwa wenyeji kurudi majumbani mwao baada ya wanyama hatari kuingia humo.

"kwa hivi sasa kuna Mamba, Nyoka na wanyama wengine hatari waliosombwa na mafuriko kwenye nyumba hizo, na huenda wakawadhuru watu na kuhatarisha maisha yao," akasema.

Muhammad amewataka wakaazi kusubiri maagizo kutoka kwa Shirika hilo pale mafuriko yatakapopungua.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.