Mashambulizi ya makombora Sudan

Imebadilishwa: 8 Oktoba, 2012 - Saa 16:27 GMT

Milima ya Nuba , Kordofan Kusini


Watu watano wameuawa na wengine 23 kujeruhiwa katika mashambulizi yaliyofanywa na waasi katika jimbo la Kordofan Kusini, kwa mujibu wa taarifa za redio ya taifa.

Mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa, alisema kuwa makombora matano yalirushwa ndani na nje ya mji mkuu wa Kordofan Kusini, Kadugli,hali iliyosababisha wafanyakazi wa kutoa misaada kukimbilia usalama wao katika maeneo ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa.

Waasi hao wamekiri kufanya mashambulizi hayo ingawa walikana kama raia walijeruhiwa.

Waasi wamekuwa wakipigana katika jimbo la Kordofan Kusini, karibu na mpaka wa Sudan Kusini , tangu mwaka jana lakini mji wa Kadugli umekuwa tulivu kwa miezi kadhaa kabla ya kuanza tena kwa vurugu hizo.

Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka jana, imekana madai ya kuunga mkono waasi hao.

Redio ya taifa, Radio Omdurman, haikusema ikiwa majeruhi walikuwa raia au wanajeshi.

Awali, jeshi la Sudan, lililaumu waasi wa SPLM-North, kwa mashambulizi hayo.

Msemaji wa jeshi la Sudan, alielezea kuwa waasi wa SPLM-North walijaribu kuingia ndani ya mji wa Kadugli na kushambulia eneo lenye umbali wa kilomita sita, Mashariki mwa Kadugli.

Umoja wa mataifa ulisema kuwa wafanyakazi wake wa misaada waliondolewa katika eneo hilo na kupelekewa katika kambi ya jeshi kama hatua ya tahadhari.

Mfanyakazi mwingine wa umoja huo alidokeza kuwa mashambulizi yalianza nyakati za asubuhi, akiongeza kuwa makombora mawili yalianguka katika makao ya shirika la UNICEF ingawa hayakulipuka.

Mapigano katika jimbo la Kordofan Kusini, yamekuwa mojawapo ya maswala nyeti ambayo yamekuwa yakichochea hali ya taharuki kati ya Sudan na Sudan Kusini katika mwaka mmoja uliopita.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.