Wanafunzi wazua rabsha Nigeria

Imebadilishwa: 10 Oktoba, 2012 - Saa 13:21 GMT

Chuo cha wanafunzi Port Harcourt

Chuo kimoja kikuu kimefungwa nchini Nigeria baada ya ghasia kuzuka kuhusiana na tukio la kuuawa kwa wanafunzi wanne, waliodaiwa kuiba komputa na simu za mkononi.

Kanda ya video ya kuogofya kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube, ilionyesha wanne hao wakiuawa kinyama.

Wanafunzi wanasema kuwa wanne hao waliuawa baada ya kudhaniwa kuwa wezi kutoka katika kijiji cha Aluu.

Chuo kikuu cha Port Harcourt (Uniport) kiliwaamuru wanafunzi kwenda nyumbani,baada ya maandamano yaliyokuwa yanafanyika kukumbwa na ghasia huku Nyumba na maduka zikichomwa.

Waandishi wa habari wanasema kuwa polisi wa kupambana na ghasia pamoja na wanajeshi, wameenda katika chuo hicho, ambacho maafisa wakuu wanasema kitasalia kufungwa hadi hali itakapotulia.

13 wakamatwa

Wanafunzi waliziba barabara moja kuu karibu na chuo kikuu kwa masaa kadhaa siku ya Jumanne na kuzuia magari kwenda ndani au kutoka nje ya mji wa Port Harcourt.

Punde wakaanza kuelekea katika eneo la Aluu, ambako wanafunzi waliuawa na genge la watu mnamo siku ya Ijumaa.

Nyumba zilizovamiwa zilikuwa za baadhi ya washukiwa wa mauaji ya wanafunzi hao.

Kanda ya video,iliyotumwa katika mtandao wa YouTube mwishoni mwa wiki, inaonyesha wanaume wanne wakivuliwa nguo na kutembezwa uchi kabla ya kuteketezwa.

Mmoja wa wanafunzi mwenzao Paul Irabor, aliambia BBC kuwa wanne hao walikuwa wameenda kuchukua pesa walizokuwa wanadai mdeni wao, wakati waliposhambuliwa kwa dhana ya kuwa wezi.

Wanafunzi hao inaarifiwa walichukua simu za mkononi na komputa baada ya mdeni wao kukosa kuwalipa ndiposa wakadhaniwa kuwa walikuwa wameiba vitu hivyo.

Watu kumi na tatu akiwemo kiongozi mmoja wa kijiji cha Aluu, ambacho kinapakana na chuo kikuu katika eneo linalojulikana kama Choba , wamekamatwa kuhusiana na mauaji hayo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.