Mlipuko wa homa ya uti wa mgongo Marekani

Imebadilishwa: 16 Oktoba, 2012 - Saa 12:27 GMT

Ukungu unaosababisha homa ya uti wa mgongo

Maafisa wa afya nchini Marekani wamesema kuwa mlipuko wa homa ya uti wa mgongo au Meningitis ambayo ilizuka mwishoni mwa wiki jana huenda iliwaathiri watu wengi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.

Walithibitisha kuwa watu 15 wamefariki kutokana na ugonjwa huo uliohusishwa na madawa ya kusisimua misuli yaliyotumiwa kutibu uchungu mgongoni.

Shirika la nchini humo la kudhibiti magonjwa, ilisema kuwa kifo cha hivi karibuni kutokana na ugonjwa huo kiliripotiwa katika jimbo la Indiana kikiwa cha pili kuripotiwa katika jimbo hilo.

Takriban watu 200 katika majimbo kumi na tatu wameathiriwa na ugonjwa huo

Kampuni moja ya madawa ililazimika kurejesha takriban makasha 17,000 ya madawa ya kusisimua misuli ambayo yalikuwa yamepelekwa katika kliniki 70 kote nchini Marekani.

Majimbo 13 yameathiriwa na homa hiyo ya uti wa mgongo, ikiwemo, Tennessee, Michigan, Virginia, Indiana, Florida, Maryland, Minnesota, North Carolina, New Jersey, Ohio, Illinois, Idaho na Texas.

Kwa mujibu wa shirika la CDC, homa hiyo siyo ya kuambukizana.

Ugonjwa wa Meningitis huathiri ubongo, na uti wa mgongo. Dalili zake huwa kuumwa sana na kichwa , kuhisi kutapika, joto mwilini na kutatizika kutembea.

Madawa hayo, yenye kusababisha homa hiyo, yanaripotiwa kutoka katika jimbo la Massachusetts.

Kampuni iliyotengeza madawa hayo, iliagiza yarejeshwe wiki jana .

Wachunguzi wa usambazaji wa madawa katika jimbo la Massachusetts, wamesema kuwa malalamiko yalitolewa dhidi ya kampuni hiyo mwaka 2002 na 2003.

Kwa mujibu wa idara ya afya ya jimbo hilo, makasha 17,676 ya dawa aina ya (Methylprednisolone acetate) yaliuzwa kwa vituo 76 vya afya, katika majimbo 23 kati ya mwezi Julai na Septemba.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.