Marekani kusaidia Lebanon kwa uchunguzi

Imebadilishwa: 22 Oktoba, 2012 - Saa 07:00 GMT

Rais wa Lebanon Michel Suleiman na waziri mkuu Najib Mikati

Marekani imesema kuwa iko tayari kuchunguza shambulizi la bomu lililomuua mkuu wa ujasusi nchini Lebanon.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali, waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton pamoja na waziri mkuu wa Lebanon Najib Mikati wamekubaliana kuhusu uchunguzi wa pamoja

Wissam al-Hassan na watu wengine saba waliuawa katika shambulio la bomu Ijumaa iliyopita.

Makabiliano yalizuka baada ya mazishi ya afisaa huyo siku ya Jumapili, huku waaandamanaji wakimtaka bwana Mikati kujiuzulu.

Mjini Beirut, Polisi waliwafyatulia risasi na gesi ya kutoa machozi waandamanaji hao walipokuwa wakijaribu kuvamia ofisi za serikali mjini humo.

Kuna ripoti kuwa huenda ghasia zaidi zikatokea Kusini na Magharibi mwa Beirut.

Viongozi wa upinzani wamelaumu nchi jirani ya Syria kwa mashambulizi hayo.

Vurugu zilizozuka siku ya Jumapili kufuatia mauaji ya Afisaa mkuu wa Ujasusi nchini Lebanon Wissam al-Hassan

Maandamano tayari yamefanyika dhidi ya Syria, nchini Leabanon na nchi washirika wake huku kukiwa na hofu ya kusambaa kwa vurugu kupitia eneo la mpakani kati ya nchi hizo mbili.

Idadi kubwa ya maafisa katika serikali ya Lebanon wanaunga mkono serikali ya Syria.

Aidha serikali ya Syria imelaani shambulizi hilo ambalo pia liliwaua walinzi wa bwana Hassan pamoja na mwanamke mmoja aliyekuwa karibu na eneo la shambulizi.

Mnamo siku ya Jumapili, Bi Clinton alisisitiza kujitolea kwa Marekani kuhakikisha uthabiti wa Lebanon, uhuru wake na muhimu kabisa usalama

Clinton ,aligusia umuhimu wa viongozi wa kisiasa kushirikiana wakati huu ili kuhakikisha hali ya utulivu inaimarishwa na kwamba wale waliohusika watawajibishwa kwa kuchukuliwa hatua za kisheria. .

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.