Bomu lauwa waumini 7 Kaduna, Nigeria

Imebadilishwa: 29 Oktoba, 2012 - Saa 11:56 GMT

Mji wa Kaduna, Nigeria

Takriban watu saba wameuawa nchini Nigeria na wengine wengi wakijeruhiwa katika shambulio la kujitoa mhanga katika kanisa la kikatoliki Kaskazini mwa Nigeria.

Maafisa wanasema kuwa gari lililokuwa limebeba mabomu liliingia katika kanisa hilo na kulipua mabomu huku athari zake zikitoboa shimo katika paa la kanisa hilo.

Shambulio hilo lilitokea mjini Kaduna, eneo ambalo limekuwa likilengwa sana na wapiganaji wa Boko Haram kwa mashambulizi katika siku za hivi karibuni.

Rais Goodluck Jonathan ameahidi kongeza juhudi za kupambana na ugaidi na vurugu nchini humo. Aidha Rais Goodluck alitaja shambulizi hilo kama kitu kisicho kubalika na ambacho kinatishia usalama na uthabiti wa nchi hiyo.

Mwandishi wa BBC mjini huko anaarifu kuwa shambulio hilo lilitokana na bomu lilotegwa kwenye gari lililopuliwa na mtu aliyejitoa mhanga na kugonga gari hilo kwenye ukuta wa kanisa.

Anasema uharibifu mkubwa ulitokea ndani ya jengo na kwamba mapaa ya maduka na nyumba za karibu yaling'oka.

Afisaa wa kanisa alisema watu kama wanne waliuwawa na wengine wengi kujeruhiwa.

Wakuu wanasema vijana wa Kikristo walioingiwa na hasira kwa sababu ya tukio hilo, walishambulia gari la serikali ambalo lilikwenda kusaidia manusura.

Kumetokea mashambulio kadha ya kidini katika jimbo hilo, mengi yamefanywa na kundi la wapiganaji wa kiislamu, Boko Haram.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.