Papa Benedict atawaza makadinali wepya

Imebadilishwa: 24 Novemba, 2012 - Saa 16:15 GMT

Papa Benedict amewatawaza makadinali sita wepya, kwenye sherehe iliyofanywa Vatikani.

Papa Benedict katika sherehe iliyofanywa Rome

Mmoja baada ya mmoja, wanaume sita kutoka Libnan, India, Nigeria, Philippines, Colombia na Marekani - walipiga magoti kuvishwa kofia nyekundu na pete ya wadhifa wao.

Mwandishi wa BBC alioko Vatikani, anasema makadinali hao wameteuliwa baada ya malalamiko kutoka viongozi wa kanisa la Katoliki katika nchi zinazoendelea, kwamba makadinali walioteuliwa awali mwaka huu walikuwa wengi wazungu, hasa Wataliana wanaotumika Vatikani.

Kwa mara ya kwanza hakuna mzungu wala Mtaliana kati ya makadinali wepya.

Lakini wazungu ndio wengi ndani ya baraza kuu la makadinali 120 ambalo ndilo humchagua papa mpya.

Mtindo unaelekea kuwa na kanisa litalowakilisha wafuasi wake ulimwenguni.

Papa aliwakumbusha makadinali wepya kwamba kofia na makoti mekundu wanayovaa ni alama kuwa wamejitolea kumwaga damu kutetea imani yao ikihitajika.

Papa Benedict piya alisisitiza kuwa Kanisa Katoliki ni la binaadamu wote wa utamaduni na makabila yote.

Uamuzi wa Papa wa kuteua makadinali kutoka nchi tatu zenye Waislamu wengi, yaani Libnan, Nigeria na India, unaonesha ana wasiwasi juu ya uhusiano baina ya Ukristo na Uislamu.

Kadinali kutoka Libnan ni kasisi wa kati ya makanisa kongwe kabisa Mashariki ya Kati.

Askofu wa Abuja, kadinali mpya kutoka Nigeria ambako nusu ya wananchi ni Waislamu, anaweza pengine siku moja kuwa papa wa kwanza kutoka Afrika.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.