Hali ya kibinadamu inazorota Goma

Imebadilishwa: 27 Novemba, 2012 - Saa 07:57 GMT

Mtoto huyu akiwa na wengine wameachwa bila makao na hapa wanasubiri kupewa chakula cha msaada

Mashirika ya misaada yametangaza kuwa hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wiki moja baada ya mji huo kutekwa na waasi wa M23 wanaopigana na serikali ya Kinshasa.

Serikali imetangaza kuwa mazungumzo yataanzishwa hivi karibuni, ili kuzingatia vipengee kadhaa vya makubaliano ya amani ambavyo havijatekelezwa.

Hapo jana kiongozi wa kisiasa wa kundi la waasi la M23 aliwasili mjini Kampala kwa mkutano na wakuu wa majeshi kanda ya maziwa makuu.

Msemaji wa kundi hilo, aliambia BBC kuwa mkutano huo utaangazia ikiwa waasi hao wataondoka katika mji wa Goma.

Waasi waliuteka mji huo, wiki jana, ingawa serikali ya Congo pamoja na nchi zingine za ukanda huo zimewasihi waasi hao kuondoka katika mji huo kama sharti la kusikilizwa kwa matakwa yao.

Waasi wa M23 ni wanajeshi walioasi jeshi la Congo mwezi Aprili , na wanasema kuwa serikali imekataa kutimiza baadhi ya makubaliano waliyoafikia mwezi Machi mwaka 2009.

Uganda imekuwa ikipatanisha waasi hao na serikali ya DRC tangu mwezi Agosti.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala Cathrene Byaruhanga anasema kuwa waasi hao wana hadi mwishoni mwa leo kuondoka Goma.

Watu wengi wamelazimika kutoka mji huo kufuatia vita

Hii ndio amri iliyotolewa na viongozi wa kikanda siku ya Jumamosi.

Majirani wa Congo, wakiongozwa na Uganda wanajaribu kuzima uasi huo Mashariki mwa nchi. Kufuatia mkutano uliofanyika mwishoni mwa Juma, viongozi wa maziwa makuu waliwasihi waasi hao kundoka Goma kabla ya kuanza kwa mazungumzo nao.

Rais Joseph Kabila, alikutana na waasi hao pia mwishoni mwa wiki lakini akasisitiza kuwa mazungumzo hayajaanza.

Waasi wanasema wangalia wanatathmini hatua za kuchukua.

Hata hivyo jeshi la Uganda lilikataa kuthibitisha ikiwa kiongozi huyo, Brigedia Generali Sultani Makenga yuko mjini Kampala.

Baraza la usalama la umoja wa Mataifa lilimwekea vikwazo vya usafiri wiki mbili zilizopita kwa sababu ya harakati za waasi hao Mashariki mwa Congo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.