Tanzania kusimamia wanajeshi wa pamoja DRC

Imebadilishwa: 7 Disemba, 2012 - Saa 16:14 GMT

Hali katika Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ni tete

Jumla ya nchi kumi katika eneo la Maziwa makuu zimekubaliana kuunda jeshi la pamoja litakalokuwa na jumla ya askari 4,000 katika kukabiliana na ghasia na vita vya mara kwa mara mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Waziri wa Ulinzi wa DR Congo, Dakta Crispus Kiyonga amethibitisha uundwaji wa jeshi hilo, akisema litafanya kazi chini ya usimamizi wa Tanzania.

Mapigano ya hivi sasa mashariki mwa Congo yalizuka mwezi Aprili mwaka huu wakati waasi wa M23 walipoliasi jeshi la nchi hiyo na kusababisha watu laki tano kuyakimbia makaazi yao wakihofia usalama wao.

Wakati huohuo, viongozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini Mwa Afrika, SADC, wameanza mkutano wao wa dharura jijini Dar es salaam nchini Tanzania.

Wameanza kwa kufanya kikao cha Asasi ya Ulinzi, Siasa na Usalama ya SADC inayojulikana kama TROIKA chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, kikao hicho cha TROIKA kimewakutanisha marais Jakaya Kikwete, Hifikepunye Phohamba wa Namibia na Jacob Zuma wa Afrika Kusini.

Amesema mara baada ya kikao hicho cha TROIKA viongozi hao watajumuika na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye pia ni mwenyekiti wa mkutano wa kimataifa wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu, pamoja na Rais Armando Guebuza wa Msumbiji ambaye ni Mwenyekiti wa sasa SADC.

Viongozi hao kwa pamoja watajadiliana kwa kina matatizo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Madagascar na Zimbabwe ambapo watawasilisha mapendekezo yao katika mkutano mkuu wa viongozi wote 14 wa SADC utakaofanyika kesho.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.