John Mahama ashinda uchaguzi Ghana

Imebadilishwa: 10 Disemba, 2012 - Saa 06:24 GMT
Wapiga kura nchini Ghana

Wapiga kura nchini Ghana

Tume ya Uchaguzi nchini Ghana imetangaza John Mahama kama mshindi wa uchaguzi wa urais. Mahama alikuwa rais kabla ya uchaguzi.

Tume hiyo ilisema kwamba Bwana Mahama alishinda kwa asilimia 50.7 dhidi ya mpinzani wake Nana Akufo-Addo aliyepata 47.74%.

Hata hivyo chama cha upinzani cha NPP kimesema kwamba kitayapinga matokeo hayo, huku kikilaumu chama tawala cha NDC kwa kupanga njama na tume hiyo ili kubadilisha matokeo ya uchaguzi uliofanyika Ijumaa.

Rais Mahama aliwasihi "viongozi wote wa vyama vyote vya kisiasa kuheshimu uamuzi wa wananchi".

"Sauti ya wananchi ni sauti ya Mungu," alisema.

Polisi mjini Accra walilazimika kufyatua vitoa machozi ili kuwatawanya wafuasi wa upinzani waliokuwa wamekusanyika nje ya ofisi za tume hiyo.

Wakati matokeo yakitangazwa, vifaru vilikuwa vikilinda ofisi za tume hiyo, na barabara zilizoizunguka zilikuwa zimewekwa vizingiti na polisi.

"Mabibi na mabwana, kulingana na matokeo tuliyopata, namtangaza John Dramani Mahama kama rais-mteule," mkuu wa tume Kwadwo Afari-Gyan aliwaambia waandishi habari.

Bwana Akufo-Addo

Bwana Akufo-Addo

Alisema asilimia 80 ya wapigaji kura walijitokeza.

Matokeo yakataliwa

Katika taarifa rasimu iliyotumwa kwa waandishi habari mnamo Jumapili kupitia barua pepe, upinzani ulisema kwamba utayapinga matokeo hayo.

"Hali hii ikikubaliwa kuendelea bila kupingawa au kusahihishwa italeta madhara makubwa kwa misingi ya taratibu za uchaguzi na hali halisi ya demokrasia nchini Ghana," NPP ilisema.

"Kukubali matokeo haya ni kuidharau demokrasia nchini Ghana, na, kwa hali hiyo hiyo, kuvuruga taratibu za kukuza demokrasia barani Afrika. Kwa minajili hii, New Patriotic Party haitayakubali matokeo ya uchaguzi wa urais kama yalivyotolewa na Tume ya Uchaguzi jioni hii."

Awali, NPP ilikuwa imesema kuwa ilikuwa na “ushahidi wa kutosha” kuthibitisha kwamba Bwana Akufo-Addo alikuwa ameshinda uchaguzi huo.

"Chama tawala cha NDC kilipanga njama na baadhi ya wafanyikazi wa EC katika maeneo bunge fulani kote nchini ili kubadilisha matokeo, na hivyo kudharau uamuzi wa wananchi wa Ghana," chama hicho kilisema.

John Dramani Mahama

John Dramani Mahama

"Ni kitendo hiki cha kuiba kura makusudi katika ngazi kulikokuwa kunafanywa mahesabu ndicho kiligundilika mapema."

Uchaguzi wa amani

Mshauri wa maswala ya kirais wa Bwana Mahama, Tony Aidoo, alisema madai hayo yalikuwa hayana ukweli wowote.

Bwana Akufo-Addo alishindwa katika uchaguzi urais wa 2008 kwa asilimia moja tu, lakini akakubali matokeo.

Matatizo ya mashine mpya za kupiga picha alama za vidole, katika maeneo kadhaa nchini, yalilazimisha uchaguzi uoendelee hadi Jumamosi.

Hata hivyo, wachunguzi walisema kwamba uchaguzi huo, kwa ujumla, ulifanyika kwa amani.

Bwana Mahama alikuwa makamu wa rais hadi rais John Atta Mills alipofariki ghafla mwezi Julai mwaka huu, ndipo akawa rais.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.