Puntland yataka komboa meli iliyotekwa

Imebadilishwa: 15 Disemba, 2012 - Saa 17:21 GMT

Wakuu katika jimbo la Somalia lilojitenga la Puntland, wanasema walinzi wa pwani wanajaribu kuikomboa meli iliyotekwa na maharamia zaidi ya miaka miwli iliyopita.

Askari wa Puntland

Meli hiyo, MV Iceberg One, iliyosajiliwa Panama, inazuwiliwa katika pwani ya Puntland eneo ambalo lina magengi mengi ya maharamia.

Serikali ya Puntland inasema jeshi litaendelea na shughuli hiyo hadi meli na mahabusu wamekombolewa.

Operesheni hiyo imeendelea kwa siku kadha.

Wakuu wanasema maharamia watatu waliuwawa Jumaane wakati wanajeshi walipokamata mashua ya maharamia iliyokuwa na shehena ya silaha na vyakula vikipelekwa kwenye meli iliyotekwa.

Vyombo vya habari vya Puntland vinasema mwanajeshi mmoja ameuwawa; wakuu wanakanusha hayo lakini wanakiri kuwa watu wao wane wamejeruhiwa.

Puntland inasema mahabusu walikuwa wanazuwiliwa sehemu mbali-mbali lakini sasa wamekusanywa kwenye meli moja.

Mashambulio ya maharamia katika pwani ya Somalia yamepungua sana katika miaka miwili iliyopita.

Wataalamu wanasema sababu ni ushirikiano kati ya majeshi ya wanamaji ya mataifa mbali-mbali yanayopiga doria katika eneo hilo na walinzi kuzidishwa ndani ya meli zenyewe.

Hata hivyo, meli kadha na mabaharia wake bado zinazuwiliwa na maharamia.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.