Wanajeshi wa Jordan waachiliwa Sudan

Imebadilishwa: 2 Januari, 2013 - Saa 14:31 GMT

Wanajeshi wa kutunza amani wa UNAMID

Wanajeshi wawili wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, waliokuwa wametekwa nyara nchini Sudan wameachiliwa huru.

Wanajeshi hao waliachiliwa baada ya kutoweka siku mia moja na thelathini na tatu ziliziopita, katika eneo la Darfur.

Msemaji wa jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa katika eneo hilo, Aicha Elbasri, amesema wanajeshi hao wako katika hali nzuri.

Amesema wanajeshi hao wawili kwa sasa wako njiani kuelekea mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum, kisha watasafiri kuelekea Jordan baada ya kuachiliwa huru katika mji kuu wa jimbo la Darfur ya Kati, Zalingei.

Wanajeshi hao wawili walitoweka tarehe 20 mwezi Agosti mwaka 2012, mjini Kebkabiya, takriban kilomita mia moja arobaini magharibi mwa El Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur ya Kaskazini, ambao Umoja wa Mataifa umeutaja kukosa hali ya usalama.

Mazungumzo ya kuwarejesha nyumbani

Idara ya polisi nchini Jordan imepongeza uamuzi huo wa kuwaachilia huru Hassan Mazawdeh na Qasem Sarhan ambao walikuwa katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa.

Wanajeshi wa kutunza amani wa UNAMID

Idara hiyo imesema kwa sasa inawasiliana na serikali ya Sudan na Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha kuwa wanajeshi hao wanarejea salama.

Taarifa za Umoja wa Mataifa zinasema kuwa askari hao walitekwa nyara wakati walipokuwa wakinunua bidhaa katika soka la Kebkabiya.

Kufikia sasa haijulikani idadi ya wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa waliotekwa nyara nchini Sudan tangu jeshi hilo kutumwa nchini humo miaka mitano iliyopita.

Kikosi cha UNAMID, nchini Sudan ndicho kikubwa zaidi katika vikosi vya Umoja wa Mataifa vilivyopo katika nchi yoyote duniani.

Wanajeshi watano wa Umoja huo nchini Sudan wameuawa, watano kati yao waliuawa mwezi Oktoba mwaka uliopita.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.