Mauaji mapya Tana River, Kenya

Imebadilishwa: 9 Januari, 2013 - Saa 08:32 GMT

Mapigano ya awali katika Tana River pia yalisababisha vifo vya watoto na akina mama

Takriban watu 8 wameuawa na wengine kujeruhiwa katika mapigano mapya eneo la Tana River kusini mashariki mwa Kenya. Taarifa hizi ni kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu

Mamia waliuawa mwaka jana katika mapigano mengine ya kikabila katika eneo hilo.

Wawili kati ya watu wanane waliouawa wanaaminika kuwa washambuliaji walioshambulia kijiji cha Orma usiku wa kuamkia leo.

Watu wengine watatu walijeruhiwa vibaya , kwa kukatwa katwa na mapanga. Inaarifiwa kuwa hali ni ya wasiwasi huku kukiwa na tetesi za kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi.

Polisi mmoja alithibitisha kuwa watu wanane waliuawa , tisa kujeruhiwa na kuwa nyumba ziliteketezwa wakati wa mashambulizi hayo.

Duru za polisi zilisema kuwa wale waliouawa ni watu kutoka jamii hizo mbili. Na idadi yao imefikisha idadi ya waliouawa tangu kuanza kwa mashambulizi haya ya kuvizia kati ya jamii hizi hadi watu 140.

Ni Chini ya miezi miwili kabla ya uchaguzi mkuuu kufanyika Kenya kwa mara ya kwanza tangu uchaguzi wa mwaka 2007 uliokumbwa na utata na kusababisha ghasia.

Ghasia hizi mpya zimesababisha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya usalama na uwezo wa polisi kuthibiti hali katika maeneo tete.

Ramani ya Kenya

Ghasia katika eneo hilo zilizuka kwa mara ya kwanza mwezi Agosti mwaka jana ambapo watu wa jamii za Pokomo ambao ni wakulima walipigana na jirani zao wa Orma ambao ni Wafugaji na kusababisha mauaji.

Mwezi Disemba pekee watu 45 waliuawa katika shambulizi lengine.

Jamii hizo zimewahi kupigana na mzozo wao umekuwa ukisemekana kusababishwa na mgogoro wa maji na malisho ya wanyama.

Lakini kwa sababu ya hali ya mashambulizi yenyewe, ambapo watoto na wanawake wamekuwa wakiuawa na nyumba kuteketezwa , imewashangaza wengi huku baadhi wakiwatuhumu wanasiasa kwa kuyachochea.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.