Wachimba migodi kukosa kazi A. Kusini

Imebadilishwa: 15 Januari, 2013 - Saa 09:36 GMT

Mwaka jana polisi waliwaua wachimba migodi waliokuwa wanagoma kudai nyongeza ya mishahara

Kampuni ya madini ya Anglo American Platinum, imesema kuwa itasitisha uzalishaji wa madini katika migodi minne eneo la Rustenberg Afrika Kusini .

Hatua hii huenda ikasababisha kuachishwa kazi kwa wafanyakazi 14,000.

Kampuni hiyo, kubwa zaidi yenye kuzalisha madini ya Platinum, imesema kuwa hitaji la chini la madini hayo pamoja na gharama kubwa ya kuyazalisha ndio chanzo cha kufungwa kwa migodi hiyo.

Amplats ilisema kuwa inapendekeza kubuni nafasi zengine 14,000 za kazi wakati itakapofunga migodi hiyo.

Mwezi Oktoba mwaka jana, kampuni hiyo iliwafuta kazi wafanyakazi 12,000 baada ya kugoma wakidai nyongeza ya mishahara.

Ilisema kuwa wakati huo migomo haramu ilisababishia kampuni hiyo hasara ya dola milioni 80. Wafanyakazi hao hata hivyo walirejeshwa kazini baadaye baada ya maafikiano kati yao na kampuni hiyo pamoja na vyama vya wafanyakazi.

Migodi kadhaa ya madini nchini humo ilikumbwa na migomo ya wafanyakazi ambapo hata wachimba migodi waliuawa na polisi.

Siku ya Jumanne kampuni ya Amplats, ilisema imeweza kudurusu mabadiliko kadhaa inayohitaji kufanya na ndio maana ikaamua kuchukua hatua hiyo.

Kampuni hiyo imesema itawalipa wale watakaoachishwa kazi

Mabadiliko hayo yataweza kuiokolea kampuni hiyo mabilioni ya dola ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015.

Kampuni ilisema kuwa mageuzi yoyote yataathiri wafanyakazi 14,000. Kati ya hawa 13,000 wako katika machimbo ya Rustenberg.

Wafanyakazi wowote au jamii zitakazoathirika kutokana na mageuzi hayo, wataweza kupatiwa msaada wa kifedha kabla ya kuachishwa kazi.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.