Armstrong kukiri haitoshi!

Imebadilishwa: 18 Januari, 2013 - Saa 14:16 GMT

Betsy Andreu, anasema alimsikia Armstrong, mwenye umri wa miaka 41, akikiri mbele ya madaktari mwaka 1996, lakini mwanamichezo huyo wakati huo alikataa kuzungumzia suala hilo.

Lance Armstrong

Amekanusha kwa miaka mingi kwamba alitumia dawa za kuongezea nguvu michezoni

"Nimesikitishwa sana", Andreu alisema katika matangazo ya CNN. Unapaswa kuniomba radhi Lance, lakini ulikataa.

"Baada ya masaibu yote yaliyonipata mimi na familia yangu, ulikataa kukiri. Na sasa tunatakikana kukuamini?"

Akionyesha gadhabu katika mahojiano, Andreu aliongezea: "Ulikuwa na nafasi ya kuelezea ukweli. Ikiwa hataki kusema ukweli, na aseme 'ndio', katika chumba cha matibabu haya yalitokea, itakuwa vipi kumwamini katika lolote lile analolisema?"

Mwandishi wa gazeti la Sunday Times, Journalist Walsh, ambaye amekuwa akimchunguza kwa muda mrefu, na aliyechangia katika kufichuliwa kwa mwanamichezo huyo, alisema mahojiano ya Oprah Winfrey hayakuwa ya kina.

Alisema Armstrong anastahili kumuomba radhi Andreu.

"Hisia zangu ni kwamba mahojiano yalikuwa sawa, lakini hayakuwa ya kina," Walsh aliielezea BBC.

"Hasa nilisikitishwa kwa yeye kukosa kukiri katika kile ambacho kingelitajwa kama hali ya kukiri katika chumba cha matibabu mwaka 1996, kwa kuwa kuna mwanamke, Betsy Andreu, ambaye mara kwa mara amekuwa akisema alimsikia akikiri kutumia dawa za kuongezea nguvu.

"Lakini kwa zaidi ya miaka kumi, ameitwa muwongo na alimhitaji Armstrong kusema maneno yake yalikuwa ya kweli, lakini alikataa kufanya hivyo."

Lance Armstrong, kwa mara ya kwanza, katika matangazo ya televisheni, amekiri kutumia dawa za kuongezea nguvu michezoni, baada ya kukanusha kwa muda wa miaka mingi, na akifanikiwa kuwa bingwa mara saba katika mashindano ya baiskeli ya Tour de France.

Katika mahojiano ya televisheni na Oprah Winfrey, alikiri kwamba kwa muda wa miaka mingi amekuwa akidanganya na kukanusha kutumia dawa hizo.

Armstrong alisema katika maisha yake yote atautumia muda wake kuendelea kuomba radhi.

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.