Mshirika wa Gbagbo afunguliwa mashtaka

Imebadilishwa: 22 Januari, 2013 - Saa 09:51 GMT

Bwana Goude anajulikana kwa hotuba zake kali alizokuwa anatoa wakati wa vurugu mwaka 2010

Waziri wa zamani wa vijana nchini Ivory Coast ambaye pia ni mshirika wa aliyekuwa rais Laurent Gbagbo, Charles Ble Goude, amefunguliwa mashtaka ya mauaji na uhalifu wa kivita pamoja na wizi wa mali ya umma.

Wiki jana bwana Ble Goude alihamishwa kutoka Ghana hadi Ivory Coast kufunguliwa mashtaka.

Bwana Ble Goude anakanusha madai kuwa waasi waliokuwa wanamuunga mkono Gbagbo walishambulia raia wa kigeni, wakati wa vurugu la baada ya uchaguzi ulliokumbwa na utata mwaka 2010.

Alitoweka mwezi Aprili mwaka 2011, wakati Gbagbo alipokamatwa.

Rais huyo wa zamani, sasa anasubiri kusikilizwa kwa kesi yake katika mahakama ya ICC, kwa makosa ya uhalifu wa kivita.

Chama cha Ivorian Popular Front (FPI), chake bwana Gbagbo, kililaani mashtaka dhidi ya bwana Ble Goude na kutaka aachiliwe mara moja ili kuboresha nafasi ya mazungumzo kati ya chama hicho na serikali.

Takriban watu 3,000 walipoteza maisha yao katika mgogoro wa kisiasa uliodumu miezi minne baada ya Gbagbo kukataa kukubali kushindwa.

Gbagbo yuko Hague akisubiri kufunguliwa mashtaka kwa kesi ya uhalifu wa kivita

Mwaka jana bwana Ble Goude, aliambia BBC kuwa kama kiongozi wa chama cha vijana cha Young Patriots aliandaa tu mikutano ya kisiasa na kuwa hakuwahi kukutana na makundi ya wapiganaji.

"mimi sio kiongozi wa wapiganaji, sijawahi kununua silaha , tulitoka kwenda barabarani kukabiliana na wale waliokuwa na silaha , hatukuwa na chochote'' alisema Ble Goude

Aliongeza kuwa yuko tayari kwenda katika mahakama ya kimataifa ya (ICC) kuweza kujiondolea lawama.

Ble Goude mwanzo aliwekewa vikwazo na umoja wa mataifa mnamo mwaka 2006, akituhumiwa kwa kuchochea mapigano dhidi ya maafisa wa Umoja huo.

Taarifa zinazohusiana

BBC © 2014 Ilani: BBC haihusiki na yaliyoandikwa na tovuti za nje ya BBC.

Ukurasa huu unaonekana vyema kwa kivinjari cha kisasa kikiwa na laha mtindo (CSS).Wakati unaweza kuona yaliyomo katika ukurasa huu kwa kivinjari ulichonacho, hautaweza kufaidi kuona kila kitu vizuri. Tafadhali zingatia uwezekano wa kuboresha progaramu ya kivinjari au kuwezesha laha mtindo (CSS) endapo unaweza kufanya hivyo.